Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amejumuika na Waumini wa Dini ya Kiislamu katika Dua Maalum ya Kumshukuru Mwenyezi Mungu pamoja na kuliombea Taifa Amani, iliyofanyika katika Msikiti wa Gombani, Mkoa wa Kusini Pemba.
Akizungumza na Waumini, Alhaj Dkt. Mwinyi amewanasihi Viongozi wa Dini na Waumini kuhimizana kulinda Amani ya Nchi na kuwa tayari kuiombea kwa dhamira ya kudumisha Utulivu.
Alhaj Dkt. Mwinyi ametumia fursa hiyo kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuijalia Zanzibar hali ya Amani na Utulivu kabla, wakati na baada ya Uchaguzi, na kuwasisitiza Waumini kuendelea kuiombea kila wanapopata fursa.
Amefahamisha kuwa kila Muumini ana daraja lake mbele ya Mwenyezi Mungu, hivyo inampasa kila mmoja kumuelekea Mungu kuomba Amani wakati wote ili aiepushe Nchi na Majanga.
Naye Katibu Mtendaji wa Afisi ya Mufti, Sheikh Khalid Ali Mfaume, amewahimiza Waumini wa Dini ya Kiislamu kufuata Miongozo ya Mtume Muhammad SAW kwa kumuomba Mwenyezi Mungu katika kila jambo linalowakabili katika maisha yao ya kila siku.
Mapema, Alhaj Dkt. Mwinyi alijumuika na Waumini wa Dini ya Kiislamu katika Sala ya Ijumaa msikitini hapo.
