Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameifungua rasmi Barabara ya Kitope–Ndagaa–Kidimni na kusisitiza kuwa ujenzi wa miundombinu ya barabara ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.Rais Dkt. Mwinyi a meyasema hayo leo tarehe 3 Disemba 2026 katika hafla iliyofanyika Kitope, Mkoa wa Kaskazini Unguja, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa bandari, viwanja vya ndege vya Unguja na Pemba pamoja na barabara kuu za mijini na vijijini, kwa lengo la kuifungua Zanzibar kiuchumi na kuiwezesha kupiga hatua kubwa ya maendeleo katika kipindi kifupi kijacho.

Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza kuwa barabara ni nyenzo muhimu ya maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla, hivyo amewataka wananchi kuitunza miundombinu hiyo na kuepuka kujenga katika maeneo ya hifadhi ya barabara.
Aidha, ametoa agizo kwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuyawekea alama zinazoonekana maeneo ya hifadhi ya barabara ili kubainisha matumizi mengine ya ziada, ikiwemo miundombinu ya maji, umeme na mawasiliano ya intaneti.

Vilevile, amewataka (ZANROAD) Wakala wa Barabara Zanzibar kuchukua hatua za awali kuzuia ujenzi holela katika maeneo ya barabara ili kuipunguzia Serikali mzigo wa kulipa fidia wakati wa upanuzi wa barabara. Rais Dkt. Mwinyi ametoa pongezi kwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa miundombinu ya barabara, pamoja na Kampuni ya ORKUN GROUP kwa kutekeleza mradi kwa viwango vinavyokubalika.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Dkt.Khalid Salum Mohamed, amesema barabara hiyo ni muhimu na italeta manufaa makubwa kwa wananchi wa eneo husika, hususan katika kuchochea ukuaji wa kilimo, usafiri na usafirishaji wa mazao ya kilimo yanayozalishwa kwa wingi na wakulima.

Akitoa taarifa ya kitaalamu ya mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Ndugu Ali Said Bakari, amesema barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 19 imejengwa na Kampuni ya ORKUN GROUP kwa gharama ya Shilingi Bilioni 33.25, fedha zilizotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.