Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuzijenga barabara zote za Mji wa Zanzibar na kuziwekea taa, kuzipanda miti maalum pamoja na njia za wanaotembea kwa miguu.Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Madiwani pamoja na Mameya kutoka Mkoa wa Mjini Magharibi.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeshatenga fedha kwa ajili ya ujenzi huo na kusisitiza kwamba baada ya ujenzi kukamilika halitokuwa tena jukumu la Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi na badala yake Manispaa ndio itakuwa na jukumu la kuzisimamia ikiwa ni pamoja na kuhakikisha zinakuwa safi.Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza kutoridhika kwake na usafi wa Mji wa Zanzibar na kueleza haja kwa wafanyakazi wa Manispaa kutekeleza majukumu yao ipasavyo katika kuhakikisha suala la usafi linapewa kipaumbele.

Aliongeza kuwa kama kuna kazi kubwa ambayo Manispaa inatakiwa kuifanya basi ni kuhakikisha Mji unakuwa safi, hivyo kuna kila sababu ya kuhakikisha mikakati ya makusudi inawekwa kwa ajili ya kuuweka Mji katika hali ya usafi.Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alisisitiza haja ya kuwepo kwa mpangilio katika Miji kwani bila ya kuwepo kwa mpangilio suala zima la usafi litakuwa gumu kutekelezeka ipasavyo.

Alisema kuwa kuwepo kwa uchafu katika Miji kunatokana na kutokuwepo kwa sheria kali za kuzuia taka na kama sheria hizo zipo basi hazisimamiwi ipasavyo wala hazifuatwi na ndio maana Miji inaendelea kuwa michafu.Rais Dk. Mwinyi alisisitiza haja ya uwajibikaji katika suala zima la ukusanyaji wa mapato sambamba na muingiliano katika shughuli zao za kazi katika Manispaa zao jambo ambalo linapelekea kutofikia malengo waliyojiwekea hasa katika makusanyo.

Hata hivyo, Rais Dk. Mwinyi aliwaeleza viongozi hao kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini jitihada zao wanazozifanya na aliwahakikishia kwamba juhudi za makusudi zitachukuliwa katika kuhakikisha changamoto zao zinazowakabili zinafanyiwa kazi.

Mapema akitoa taarifa ya Madiwani wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Jiji la Zanzibar Mahmoud Mohammed Mussa alitoa shukurani kwa Rais Dk. Mwinyi kwa kuwapatia maelekezo pamoja na miongozo kwa kupitia viongozi wao lakini zaidi kwa mchango wake mkubwa kwa Wajasiriamali pamoja na ujenzi wa miradi ikiwemo masoko, vituo vya afya na skuli kwa Unguja na Pemba.

Akieleza miongoni mwa changamoto zilizopo katika suala zima la usafi alisema kuwa ni pamoja na utunzaji wa mazingira, ukosefu wa vifaa vya kufanyia usafi pamoja na uwajibikaji wa jamii kutojuwa jukumu la usafi na ndio maana juhudi walizichukuwa za kupata vifaa vya usafi kutoka kwa wadau mbali mbali.Mstahiki Meya huyo wa Jiji alikiri kwamba bado Jiji la Zanzibar halijawa na haiba nzuri inayotakiwa hata hivyo, mabadiliko baadhi ya sehemu yameanza kuonekana na kuahidi kuendelea kushirikiana na kuleta mabadiliko kama ilivyo Miji mengine ya nje ya Zanzibar.

Hata hivyo, viongozi hao katika taarifa yao walieleza haja ya kupatiwa asilimia kadhaa kupitia Manispaa zao au kupatiwa maeneo ili Baraza liweze kujipatia vyanzo vya mapato.Sambamba na hayo, viongozi hao walieleza matarajio yao makubwa baada ya kukamilika kwa mradi wa maduka ya Darajani Bazar, na kutoa pongezi kwa Rais Dk. Mwinyi kwa juhudi anazozichukua katika kubuni miradi mbali mbali ya maendeleo hapa nchi.

Pia, viongozi hao walieleza haja ya kuwepo kwa mashirikiano ya pamoja katika masoko ya muda yanayotoa huduma kwa wananchi hivi sasa huku kukisubiriwa kukamilika kwa masoko mapya ambayo yataongeza mapato sanjari na kuongeza ajira kwa vijana.