MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza dhamira yake ya kuzihuisha mali zinazomilikiwa na chama cha Mapinduzi (CCM) kwa lengo la kukiendeleza chama hicho.Dk. Mwinyi aliyasema hayo alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua mali za CCM zilizopo maeneo mbalimbali ya Chama kwa Unguja.
Alieleza kwenye ziara yake hiyo yakutembelea majimbo mbalimbali ya chama, anaangalia fursa zilizopo sehemu hizo na kuona jinsi ya kuwekeza kibiashara ili kukiinua chama kiuchumi.Makamu Mwenyekiti huyo alieleza ndani ya kipindi kifupi cha uongozi wake, anatarajia kukiona chama kinawekeza kwa vitendo miradi mbalimbali ya uwekezaji ili isaidie kukiimarisha chama hicho.
Pia aliwataka wanachama wa CCM kuiendeleza miradi iliopo wakati mengine inayotarajiwa kuanza hivi karibuni kwa nia ya kuimarisha nguvu chama kimkakati na uchumi pamoja na kuziboresha ofisi za chama hicho kuendelea kuwa na hadhi ya Chama.Akizungmza kwa nyakati tofauti wakati akiorodhesha mali za chama hicho, Katibu wa Kamati Maalum NEC, Idara ya Uchumi na Fedha kutoka ofisi Kuu ya cha Chama, Kisiwandui, Afadhali Taibu Afadhali, aliyataja maeneo ya kimkakati yanayomilikiwa na chama hicho ikiwemo eneo la tawi la CCM Mbweni, ukumbi wa CCM Maisara Social Hall, nyumba ya kumbukumbu ya Afro - Shiraz iliopo eneo la Posta ya Kijangwani pamoja na eneo la kituo cha mafuta, sheli ya Kinazini, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Ziara hiyo ya Makamu Mwenyekiti wa CCM, Zanzibar ni mwendelezo wa ziara zake ndani ya Chama kwa kuzitembelea ofisi za chama hicho kwa ngazi zote ikiwa ni utekelezaji wa majukumu yake ndani ya chama na kukagua mali zinazomilikiwa na Chama kwa ngazi zote.