Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza kwamba ushirikiano na uhusiano ulioahidiwa kuimarishwa na nchi za Saudi Arabia, Indonesia na Jamhuri ya Watu wa Kenya una tija kubwa katika kukuza sekta za maendeleo hapa Zanzibar.Rais Dk. Mwinyi amesema hayo leo Ikulu Zanzibar mara baada ya kufanya mazunguzo na Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania Abdullah Bin Ali Alsheryan, Balozi wa Indonesia nchini Tanzania Tri Yogo Jatmiko pamoja na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa Kenya Dan Kazungu alipokutana nao kwa nyakati tofauti.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi aliipongeza Saud Arabia kwa azma yake ya kuendelea kushirikiana na kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo kupitia Taasisi yake ya “Saud Fund”.Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha sekta za maendeleo hapa nchini hasa ikizingatiwa kwamba nchi hiyo imeanza kuisaidia Zanzibar kwa muda mrefu.
Alisema kuwa ahadi ya nchi hiyo ya kuleta madaktari bingwa wa upasuaji hapa Zanzibar kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi kutasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha sekta ya afya hapa nchini.Aidha, Rais Dk. Mwinyi alimueleza Balozi Alsheryan kwamba Sera ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hivi sasa ni kuimarisha Uchumi wa Buluu hivyo, Saud Arabia inakaribshwa katika kuimarisha Sera hiyo hasa ikizingatiwa kwamba fursa kadhaa bado zipo.
Kwa upande wa Jamhuri ya Watu wa Kenya, Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi kwa nchi hiyo kwa kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo ambao amesisitiza kwamba Zanzibar itaendelea kuuimarisha kwa manufaa ya pande zote mbili.Alieleza kwamba hatua ya Jamhuri ya Watu wa Kenya kuifanya Zanzibar kuwa mwenyeji wa mkutano wa Mawaziri wa Jamhuri ya Kenya na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utakaofanyika Machi 9,2022 ukiwa na azma ya kujadili masuala mbali mbali yakiwemo yale ya kibiashara kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuleta manufaa kwa pande zote mbili.
Alimpongeza Balozi wa Jamhuri ya Watu wa Kenya anaemaliza muda wake wa kazi hapa nchini Dan Kazungu kwa kutekeleza vyema kazi zake wakati wote alipokuwa hapa nchini na kuwa na mahusiano mazuri kati yake na viongozi pamoja na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Katika mazungumzo kati yake na Balozi wa Indonesia nchini Tanzania Tri Yogo Jatmiko, Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa Indonesia ni mdau mkubwa wa Zanzibar katika biashara ya karafuu sambamba na uimarishaji wa zao hilo.
Rais Dk. Mwinyi alipongeza utayari wa nchi hiyo wa kuliongeza thamani zao la karafuu hapa Zanzibar kwa kulisarifu na hatimae kupata malighafi ambayo ni mafuta yatakayouzwa nje ya nchi na kuifanya Zanzibar kuwa kituo kikuu cha biashara hiyo katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.Mbali na zao hilo la karafuu, Rais Dk. Mwinyi alimueleza Balozi Jatmiko kwamba Zanzibar iko tayari kushirikiana na Indonesia katika kuendeleza na kuimarisha sekta ya uvuvi pamoja na kushirikiana katika kuwasaidia wakulima wa zao la mwani ili kulipa thamani zao hilo pamoja na kulitafutia soko kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wa zao hilo.
Nao Mabalozi hao kwa nyakati tofauti walimueleza Rais Dk. Mwinyi azma zao za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza maendeleo ya kiuchumi hapa nchini.Mabalozi hao walipongeza kasi ya maendeleo iliyofikiwa Zanzibar sanjari na mikakati iliyowekwa na Serikali anayoiongoza Rais Dk. Mwinyi jambo ambalo limewapa hamu ya kuendelea kuiunga mkono Zanzibar.
Sambamba na hayo, Mabalozi hao walieleza kufarajika kwao na ukaribu, mapenzi na mshikamano wa wananchi wa Zanzibar mambo ambayo yameijengea sifa kubwa Zanzibar za Kimataifa na Kitaifa.