Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza kwamba Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano kati yake na Oman na kuishauri nchi hiyo kuunga mkono Sera ya Uchumi wa Buluu ambayo ndio Dira ya uchumi wa Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Sayyid Badr bin Hamad bin Hamood Al Busaid akiwa amefuatana na ujumbe wake.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alimueleza Waziri Al Busaid kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini uhusiano na ushirikiano wa kihistoria kati yake na Oman hivyo, inawakaribisha wafanyabiashara, wawekezaji na wenye viwanda wa nchi hiyo kuja kuekeza Zanzibar hasa katika sekta za uchumi wa Buluu.

Rais Dk. Mwinyi alimuleza Waziri huyo kwamba Zanzibar ina fursa nyingi za kuekeza hasa katika Uchumi wa Buluu ambao ndio Dira ya uchumi wa Zanzibar hivi sasa.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Serikali ya Oman kwa kuendelea kuisaidia Zanzibar katika sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo sekta ya elimu ambapo nchi hiyo kwa muda mrefu imekuwa ikitoa ufadhili wa masomo kwa Wazanzibari na kusisitiza haja ya kuendelezwa.

Rais Dk. Mwinyi alimueleza Waziri huyo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatoa pongezi zake za dhati kwa Serikali ya Oman kwa kuunga mkono juhudi za kuutunza na kuuendeleza Mji Mkongwe wa Zanzibar kwa azma yake ya kusaidia ujenzi wa jumba la Baet el Jaib na jumba la Wananchi Forodhani ili ubaki katika haiba yake ya kuwa urithi wa dunia.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alipongeza juhudi za Serikali ya Oman kwa kuiunga mkono Zanzibar katika sekta ya uwekezaji ambapo tayari Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshatiliana saini na Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman katika miradi mikubwa miwili ukiwemo mradi wa ujenzi wa bandari ya Mangapwani pamoja na mradi wa ujenzi wa bandari ya Malindi.

Hata hivyo, katika mazungumzo hayo Rais Dk. Mwinyi alieleza haja ya kufanywa uharaka katika utekelezaji wa miradi hiyo ili lengo lililokusudiwa liweze kufikiwa.

Rais Dk. Mwinyi pia, alimueleza Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Oman kwamba ziara yake hiyo hapa Zanzibar itazidi kupanua uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya pande mbili hizo.

Nae Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Sayyid Badr bin Hamad bin Hamood Al Busaid alieleza azma ya Serikali ya Oman ya kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kidugu uliopo baina ya pande mbili hizo.

Waziri huyo wa Mambo ya Nje alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba Serikali ya Oman iko tayari kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kukuza uchumi wake kupitia Sera yake ya Uchumi wa Buluu huku akiahidi hatua zitakazochukuliwa kuhakikisha miradi iliyosainiwa inatekelezwa kwa haraka.

Aidha, Waziri Al Busaid alieleza kwamba Oman inathamani sana uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na Zanzibar hasa kutokana na kushabihiana kwa tamaduni za pande mbili hizo.

Pamoja na hayo, Waziri Al Busaid alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba Serikali ya Oman itahakikisha inakuwa Balozi wa Zanzibar kwa wawekezaji, wafanyabiashara na wenye viwanda wa nchi hiyo kuja kuekeza Zanzibar katika sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo sekta ya uchumi wa Buluu.

Sambamba na hayo, Waziri huyo alizipongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuutangaza pamoja na kuvitunza vyanzo vya utalii wa Zanzibar na kueleza kwamba nchi yake itaendelea kuunga mkono juhudi hizo.