RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza matumaini yake makubwa katika kuimarisha mashirikiano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni pamoja na kukuza sekta ya mawasiliano.Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo wakati alipofanya mazungumzo na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Moses Nnauye Ikulu Zanzibar akiwa amefuatana na ujumbe wake.

Katika mazungumzo hayo Rais Dk. Mwinyi alimpongeza Waziri Nape kwa kupata wadhifa huo na kuahidi kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza ushirikiano uliopo ili kuweza kufanikisha kuwapatia wananchi wote mawasiliano sambamba na kushirikiana katika nyanja nyengine muhimu zilizokuwemo katika Wizara hiyo ili pande mbili hizo ziweze kwenda kwa pamoja katika maendeleo.Alieleza kwamba kuweko kwa mradi wa kusambaza minara ambao itawekwa minara ipatayo 42 katika Shehia zipatazo 38 Unguja na Pemba kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuweza kuwapatia mawasiliano bora wananchi, mradi utakao simamiwa na Mfuko wa Mawasilano kwa wote (UCSAF) ulioanzishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nae Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Moses Nnauye kwa upande wake aliahidi kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kueleza kwamba ushirikiano uliopo kati ya Mfuko wa Mawasiliano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni mzuri.Alisema kwamba mradi huo utafanyika kwa kiasi ya TZS Bilioni 6.9, ambao pia, umezingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), pamoja na maelekezo aliyoyatoa katika ziara zake alizozifanya katika mikoa ya Zanzibar ambapo iligundulika kwamba kuna baadhi ya maeneo katika visiwa vya Unguja na Pemba hawapati mawasiliano bora ya simu.

Sambamba na hayo, Waziri Nape alimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba Wizara anayoiongoza itatoa mashirikiano ya kutosha hasa kwa kutambua kwamba ni Wizara ya Muungano.
Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi aliongoza aliwaongoza mamia ya wananchi katika maziko ya aliekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Marehemu Said Bakar Jecha, yaliofanyika kijijini kwao Fumba, Wilaya Magharibi ‘B Unguja.

Marehemu Said Bakar Jecha, ambae wakati wa uhai wake pia alikuwa Kamishna wa Tume ya Maadili Zanzibar, alifariki dunia jana nyumbani kwake Mazizini baada ya kuugua kwa kipindi kirefu.Marehemu Jecha, ameacha kizuka na watoto wawili atakumbukwa kwa mchango mkubwa aliotoa katika kuiendeleza SUZA kitaaluma, miundombinu pamoja na rasilimali watu katika vipindi viwili akiwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho.

Mapema, Rais Dk. Mwinyi alipata fursa ya kutoa mkono wa pole kwa ndugu na jamaa wa Marehemu na hatimae kushiriki katika Sala ya maiti iliofanyika katika Mskiti wa Ijumaa kijijini hapo.Katika maziko hayo Viongozi mbali mbali wa Kitaifa walishiriki, akiwemo Rais Mstaafu wa Zanzibar Awamu ya Sita Amani Abeid Karume, Kaimu Jaji Mkuu wa Zanzibar Khamis Abdalla Shaaban, Mawaziri, Viongozi wa Vyama vya Siasa.

Mola ailaze roho ya Marehemu mahala pema Peponi, Amin.