Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameiagiza Wizara ya Afya kuweka maduka binafsi ya dawa kwenye hospitali zote za Umma ili kuwaondoshea wananchi changamoto ya kukosa dawa ndani hospitali za Serikali. Aidha, aliwaagiza kuweka bajeti ya kutosha na kuwalipa kwa wakati ili kuepusha malalamiko kwa watoa huduma hizo.
Aliyasema hayo kwenye sherehe za ufunguzi wa hospitali ya Wilaya ya Kitogani, Mkoa wa Kusini Unguja ikiwa ni mwendelezo wa kusheherekea miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar.Dk. Mwinyi aliseama kufanya hivyo ni kuondosha dhana na malalamiko ya wananchi kwamba hospitali za serikali hazina dawa na badala yake wagonjwa kuamuriwa wakanunue dawa nje ya huduma za umma.
Alisema sekta ya Afya Zanzibar ameifanyia mabadiliko makubwa ili kurejesha imani za wananchi kwa serikali yao haswa wanapofuata huduma kwenye hospotali za Umma.
Rais Mwinyi aliekeza sasa hakuna mwananchi atakaefika kwenye hospitali ya Umma akakosa dawa au vipimo na kwamba serikali yao ya Mapinduzi ya Zanzibar imeboresha huduma za kisasa na zinapatikana wakati wote.
Aliongeza hospitali ya Wilaya Kitogani ni mfano halisi wa hospitali anazozitaka kwaaajili ya kuwahudunia wananchi wa Unguja na Pemba ili waendani na hadhi ya miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar.Akizungumzia dhana ya kushirikana na taasisi binafsi katika kutoa huduma za afya, Dk. Mwinyi alisema sio kila jambo lazima yafanywe na serikali na badala yake sekta binafsi zitasimama kuwahudumia wananchi ikiwemo huduma za maabara na vipimo kama X – ray, Ultrasound na BCG.
Alisema ndani ya hospitali ya Wilaya, Kitogani kuna taasisi binafsi iliyoingia mkataba na serikali wa kutoa huduma zote za vipimo vitakavyohitajiwa kuwatibu wananchi, nakueleza tayari wameweka vifaa vyao kwaajili ya kutoa huduma.Alisema kwa ushirikiano huo hakuna mwananchi atakaefika hospitalini hapo akakuta kifaa kibovu nakuongeza kuwa huduma zote za kisasa zitapatikana hospitalini hapo, hivyo, aliwataka watendaji wa wizara ya afya pamoja na madaktari kuhakikisha wanatoa huduma na zinazoendana na hadhi ya hospitali hiyo.
“Mwisho wa siku tutawasikiliza wananchi, baada ya muda tutawasikiliza wanasemaje, je! Jengo letu linafanana na huduma zetu?, tukipata jibu la huduma bora, basi dhamira yetu itakua imetimia, nakuombeni tuwe pamoja katika hili?” alieleza Dk. Mwinyi.Hata hivyo, alisisitiza suala la usafi na mwonekano mzuri kwa mandhari yote ya hospitali na kuwaeleza watakao ajiriwa kwenye sekta hiyo kutimiza wajibu wao, ili kuondokana na dhana ya uchafu kwa hospitali za serikali.
Katika hatua nyengine, Dk. Mwinyi aliziagiza serikali za Mkoa na Wilaya ya Kusini washirikiane na halmashauri ya Mkoa huo kuwawekea mazingira mazuri wafanyabiashara wadogo watakaotoa huduma kwenye hospitali hiyo na kuwawekea utaratibu utakaoleta taswira njema kwa hospitali.
Naye, Makamo wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla aliwataka wahudumu wa afya kwenye hospitali hiyo kuwajibikaji na kujitoa kwenye majukumu yao ili kubadili mitazamo potofu kwa jamii. Aidha, alieleza kufunguliwa kwa hospitali hiyo kunatekeleza ilani ya CCM kwa kutekeleza miradi ya maendeleo nchini na kueleza kwamba hospitali ya Kitogani ni ya pili kufunguliwa na Mhe. Rais ikiwemo ile wa Wilaya ya Micheweni aliyoizindua Januari 03 mwaka huu.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Afya Nassor Ahmeid Mazrui, aliwaagiza Mbunge na Mwagilishi wa jimbo la Paje kuwajengea kituo cha daladala wagonjwa na wananchi wanaofika hospitalini hapo na kuwataka ndani ya kipindi cha miezi miwili wakamilishe ujenzi huo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu kuu kutoka Wizara ya Afya, Amour Suleiman Muhammed alisema hospitali inauwezo wa kulaza hadi wagonjwa 100 kwa wakati na kuhudumia wananchi 52, 850 wakiwemo maeneo jirani na kuongeza kuwa inatoa huduma za wagonjwa wa nje (OPD), huduma za mama na mtoto, kiliniki za pua, koo na masikio, magonjwa yasioambukiza ikiwemo kisukari, sindikizo la damu, huduma za dawa, ushauri nasaha na kupinga vitendo vya udhalilishaji, huduma za uchunguzi wa maabara na vipimo
Aidha, alieleza hospitali ina wodi ya watoto, wodi ya mama wajawazito wa kabla na baada ya kujifungua, wodi ya watu wazima wanaume, (ICU) ya watoto na ya watu wazima, huduma za watoto njiti na wodi tatu za wagonjwa wenye mahitaji maalum ya kujitenga, aliongeza kuwa hospitali hiyo itaondosha msongamano kwenye hospitali kuu ya Mnazi Mmoja badala yake wagonjwa kutoka hospitali ya Makunduchi na maeneo mengine ya mkoa huo watahudumiwa na hospitali hiyo.
Hospitali ya Wilaya Kitogani ni miongoni mwa hospitali 11 za miradi ya Wizara ya Afya zikiwemo 10 za Wilaya na Moja wa Mkoa zinazojengwa na Serikali ya awamu ya nane kwa fedha za ahuweni ya uviko 19 Zanzibar. Ilianza ujenzi Disemba 23 mwaka 2021 kwa gharama za silingi bilioni 6.894 na shilingi bilioni 1.780 zilikadiriwa ununuzi wa vifaa tiba na milioni 164.527 zilinunuliwa gari la kubebea wagonjwa hadi kukamilika kwake ilitumia shilingi bilioni 8.839.