Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kusitisha mkataba wa Kampuni ya MBH Hydrotech Co. Ltd inayojenga vyoo vya skuli za Mkoa wa Kaskazini Unguja na badala yake kazi hiyo wapewe kikosi cha Mafunzo.Rais Dk.Mwinyi ametoa agizo hilo leo huko katika viwanja vya skuli ya Msingiya Mkwajuni Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja mara baada ya kuweka mawe ya msingi katika uzinduzi wa madarasa katika skuli ya Msingi na ya Sekondari ya Mkwajuni.

Uamuzi huo umekuja baada ya kuonekana uwezo wa Kampuni hiyo ya MBH Hydrotech Co.Ltd ya Zanzibar kuwa mdogo hatua ambayo imepelekea kukengeuka masharti ya ujenzi huo na kuona haja ya kuvunja mkataba na Kampuni hiyo inayojenga vyoo 338 vya skuli katika Mkoa wa Kaskazini Unguja kupitia fedha za UVIKO-19.Katika maelezo yake, Rais Dk. Mwinyi aliendelea kusisitiza kuwa hakuna haja ya kubembelezana na Kampuni ambazo zimeshindwa kutekeleza masharti ya ujenzi waliopewa na kueleza kwamba kikosi cha Mafunzo kinaweza kufanya kazi hio.

Rais Dk. Mwinyi alikipongeza kikosi cha Mafunzo kwa kukamilisha vyema ujenzi wa madarasa 10 yakiwemo 7 mapya ya Msingi na 3 ya Sekondari yaliyokamilishwa.Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba baada ya kumalizika kwa fedha za UVIUKO 19 zinazojenga miradi kadhaa hapa nchini Serikali itatafuta fedha nyengine kwa ajili ya miradi mengine ya maendeleo.Aliendelea kueleza kwamba kipaumbele kitatolewa zaidi katika suala la ajira kwa wale waliojitolea hasa pale ajira hizo zitakazpotangazwa.

Rais Dk. Mwinyi aliutaka uongozi wa Mkoa kuhakikisha unaingia katika ushindani na Mikoa mengine katika masomo ili waendelee kwua na matokeo mazuri hasa ikizingatiwa kwamba Serikali inajitahidi kuweka miundombinu.

Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Lela Mohammed Mussa alieleza jinsi Mkandarasi wa Kampuni ya MBH Hydrotech Co.Ltd anavyosuasua katika ujenzi huo na kupelekea kutofikiwa malengo yaliyokusudiwa.

Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wa Mkoa huo kwa upande wao walimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa utekelezaji wake wa Ilani ya Uchaguzi kwa vitendo.

Mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha Wajasiriamali cha Pale Kiongele katika Jimbo la Tumbatu, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa lengo la Serikali ni kuwa na vituo vingi vya namna hiyo ikiwa ni pamoja na kujenga masoko ya kisasa ya samaki katika Mikoa ya Unguja na Pemba ili kuweka mazingira mazuri ya wajasiriamali.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi aliyataka Mabaraza ya Miji kutafuta fedha na kujenga vituo kama hivyo ili wajasiriamali waweze kupata fursa ya kufanya shughuli zao vizuri.

Pia, alikipongeza kikosi cha Chuo cha Mafunzo kwa kujenga jengo hilo kwa gharama nafuu na kwa wakati hali ambayo imemridhisha na juhudi za kikosi hicho.

Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba bado fedha zipo za kutosha hivyo ni vyema Wajasiriamali wakatumia fursa hiyo na kuwataka kuwa na utamaduni mzuri wa kurejesha mikopo ili waweze kuongezewa zaidi pamoja na wengine kufaidika.

Akiweka jiwe la msingi katika hospitali ya Wilaya ya Kaskazini A, huko Kivunge, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba lengo la Serikali ni kuhakikisha kila Wilaya inakuwa na hospitali ya kisasa pamoja na vifaa vikiwemo vifaa tiba pamoja na wataalamu.

Alieleza azma ya Serikali ya kutoa kibali cha ajira ambapo Wizara ya Afya pamoja na Wizara ya Elimu nazo zitafaidika na ajira hizo hatua ambayo itapunguza changamoto ya utoaji huduma za afya kwa wananchi.

Alisema kuwa huduma nyingi zikiwemo za upasuaji zitatolewa hapo hapo katika hospitali hizo za Wilaya ikiwemo hospitali hiyo ya Wilaya ya Kaskazini A, iliyopo Kivunge huku akiwahakikishia wafanyakazi wa sekta hiyo maslahi bora ili na wao watoe huduma bora.

Rais Dk. Mwinyi alieleza hatua zilizochukuliwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), katika kuhakikisha inapata pampu za maji nne za zarura kwa azma ya kupeleka huduma ya maji kwa baadhi ya wananchi wanaokosa huduma hiyo hivi sasa baada ya pampu zao kuungua.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alipokea ombi la kujengwa kwa barabara ya kijini na kueleza hatua zitakazochukuliwa katika kuhakikisha utekelezaji wake unafanyika kwa kupitia Mradi wa Barabara za Vijijni.

Mkuu wa Mkoa huo Ayoub Mohammed Mahmoud nkwa upande wake alitoa pongezi kwa Rais Dk. Mwinyi kwa juhudi zake za kuwapelekea maendeleo wananchi wa Mkoa huo.

Mapema Rais Dk. Mwinyi alipokea taarifa ya Utekelezaji wa shughuli za maendeleo za Mkoa wa Kaskazini Unguja huko katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.