RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameishukuru Jumuiya ya Ulaya (EU) kwa Zanzibar kuwa miongoni mwa maeneo yatakayopata misaada kutoka Jumuiya hiyo kwa ajili ya kuendeleza miradi mbali mbali ya Maendeleo.Dk. Mwinyi ametoa shukrani hizo alipozungumza na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji Jestas Abouk Nyamanga , aliefika Ikulu Zanzibar kwa kujitambulisha pamoja na mazungumzo mafupi.

Amesema ni jambo jema kwa Zanzibar, hususan kisiwa Cha Pemba kuwa miongoni mwa maeneo ambapo miradi mbali mbali ya maendeleo itatekelezwa chini ya Ufadhili wa EU hapa Tanzania, ikiwemo mradi wa ‘kuboresha mtazamo wa Majiji’ (green City), ambao unakusudiwa kutekelezwa katika miji mitatu ya Tanzania ya Tanga, Mwanza na Pemba.Alisema tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya nane, yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa (GNU), kumekuwepo dalili za EU kurejesha Uhusiano wake na Zanzibar kufuatia kuwepo kwa Demokrasia.

Aidha, Dk.Mwinyi alieleza kuwa Utalii ni sekta kuu ya Uchumi wa Zanzibar, na kusema Zanzibar imejipanga kuimarisha sekta hiyo baada ya kuathirika kutokana na Ugonjwa wa Covid-19.Alimtaka Balozi huyo kuendeleza mazungumzo na mamalaka zinazosimamia Utalii nchini Ubelgiji ili kufanikisha lengo la kuwepo safari za ndege za moja kutoka Ubelgiji hadi Zanzibar na hivyo kuleta matumaini ya kuongeza ujio wa Watalii hapa nchini.

Akigusia suala la kuwepo fursa za Biashara nchini Ubelgiji, Dk. Mwinyi alisema Diplomasia ya Uchumi inazingatia umuhimu wa kuangalia fursa za biashara, hivyo akasema pamoja na kuwepo changamoto mbali mbali katika utayarishaji wa Dagaa kwa wajasiriamali hapa nchini, Serikali itaishughulikia changamoto hiyo hatimae fursa hiyo iweze kutumika ipasavyo.Alisema Zanzibar imekuwa ikishughulikia miradi mbali mbali kwa ajili ya maendeleo, hivyo kuwepo kwa taasisi zinazotoa mikopo nafuu ni jambo jema na kubainisha namna Serikali itazingatia namna itakavyoweza kupata mikopo hiyo kupitia mashirika hayo ya Fedha yaliopo EU.

Aidha, alisema Zanzibar itashukuru kupata fedha za mkopo kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu kupitia sekta ya uchumi wa Buluu.

Mapema Balozi wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania nchini Ubelgiji, ambapo pia anaiwakilisha Tanzania nchini Luxenbourg na Jumuiya Umoja wa Ulaya (EU Jestas Abouk Nyamanga amesema kuanza kwa safari za moja kwa moja za ndege kati ya Ubelgiji na Zanzibar kuanzia mwezi Oktoba mwaka huu, kutaongeza idadi ya Watalii watakaozuru nchini.Alisema mawasiliano yamefanyika kuona kunakuwepo usafiri wa ndege ya moja kwa moja kati ya Ubelgiji – Zanzibar kwa wastani wa mara mbili kwa wiki na hivyo kuongeza idadi ya ujio wa Watalii baada ya kuathirika kutokana na Ugonjwa wa Covid -19, ambapo kabla ya ugonjwa huo wastani wa watalii 16,000 walikuwaa wakizuru nchini kila mwaka.

Alisema katika mazingira ya sasa Watalii kutoka nchi hiyo hutumia Shirika la Ndege la Qatar, jambo ambalo lina changamoto mbali mbali.

Aidha, alisema nchi hiyo ina fursa mbali mbali za msomo ya juu, hususan katika kiwango cha Master na PHD, hivyo akatoa wito kwa Vyuo vikuu vya Zanzibar,  ikiwemo SUZA pamoaj na wananchi wengine wenye uwezo kuhamasika ili kutumia fursa ziliopo.Balozi Nyamanga alisema mahusiano kati ya Tanzania na Ubelgiji yameimarika na kubainisha fursa kadhaa za kibiashara, ambapo Tanzania inaweza kufanya, ikiwemo kuuza minofu ya samaki, dagaaa, mbogamboga, mchele pamoja na viungo vya aina mbali mbali.

Alisema Zanzibar inaweza kunufaika na fursa hiyo kupitia uuzaji wa Dagaa, mkazo ukiwekwa katika utayarishaji na uhifadhi bora wa dagaa hilo ili kuliongezea thamani, pamoja na usafirishaji wa viungo ikiwemo Pilipili.Kuhusiana na Uwekezaji, Balozi Nyamanga alisema Luxembourg ni kituo kikuu cha Mashirika ya Fedha pamoja na Mabenki , huku akibainisha kuwepo Kampuni zinazoonyesha nia ya kutoa mikopo nafuu kwa Zanzibar, hivyo akaiomba Serikali kubainisha maeneo yanayoweza kutumika.

Akizungumzia mahusiano ya Tanzania na Jumuiya Umoja wa Ulaya, Balozi Nyamanga alisema kuwa ni mazuri, ambapo EU imekwua ikiendelea kutoa misaada, hususan ya kifedha kwa Tanzania.Alisema EU imetenga kiasi cha Euro Milioni 554 kwa Tanzania ili kuiwezesha kuingia katika soko la Ulaya pamoja na Euro Milioni kumi kwa ajili ya kuimarisha uzalishaji wa Asali ya Nyuki.

Aliitaja mikoa ya Katavi, Rukwa, Tabora, Dodoma na Pemba kuwa itanufaika na msaada huo, lengo likiwa ni kuzalisha asali yenye viwango .

Aidha, alieleza kuwa katika kipindi cha mwaka 2021 – 2027 EU imeahidi kusaidia Tanzania kiasi cha Euro Milioni 425, ambapo Euro Milioni 703 zimelengwa katika uboreshaji wa mitazamo ya Majiji (green city) katika miji mitatu ya Tanga, Mwanza pamoja na Pemba.Alisema fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kuimarisha miundo mbinu pamoja na masoko katika miji hiyo.

Aidha, Balozi huyo aliishukuru Serikali kwa kutilia mkazo   uimarishaji wa sekta ya Uchumi wa Buluu, akibainisha kiasi cha Euro Milioni 140 zilizotengwa na Jumuiya hiyo kwa ajili ya uimarishaji wa Uchumi wa Buluu ambapo miongoni mwa matumizi yake yatahusisha mikopo kupitia Sekta binafsi.

WAKATI HUO HUO; Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi alikuwa na mazungumzo na Balozi wa Ethiopia nchini Tanzania Shibu Mamo Kedida.Katika mazungumzo hayo yaliofanyika Ikulu Zanzibar viongozi hao walizungumzia haja ya kuendeleeza mahusiano na mashirikiano ya kihistoria kati ya Zanzibar na Ethiopia katika njanja mbali mbali kwa maslahi ya Mataifa hayo na wananchi wake.

Miongoni mwa maeneo ya mashirikiano yaliogusiwa ni pamoja na Utalii, Michezo, utamaduni, masuala ya Anga pamoja na elimu.