RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi ameishukuru Timu ya Madaktari wabobezi kupitia Mashirika ya Peleks na Direct Aid Zanzibar kwa kuanzisha utaratibu wa kuja Zanzibar kusaidia huduma za tiba.Dk. Mwinyi ametoa shukrani hizo Ikulu jijini Zanzibar wakati alipoagana na Timu ya Madaktari wabobezi kutoka Mashirika Peleks na Direct Aids Zanzibar,  waliokuja nchini kwa ajili ya kusadia utoaji wa huduma za Afya.

Madaktari hao wabobezi kutoka nchi za Saudi Arabia, Sudan, Misri na Romani wamefika nchini Mei 07, 2022 na kutoa huduma hadi Mei 14, mwaka huu katika Hospitali za Chake chake na Wete Pemba, ambapo jumla ya Operesheni za magonjwa mbali mbali 190 zilifanyika.Akizungumza na madaktari hao Dk. Mwinyi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamin juhudi na mchango mkubwa wa wataalamu hao kwa kuzingatia kazi kubwa na nzuri waliyofanya kusaidia uimarishaji wa afya za wananchi kisiwani Pemba.

Alisema hatua hiyo imesaidia Serikali kupunguza gharama za kusafirisha wagonjwa nje kwa ajili ya rufaa.Alifahamisha hatua iliochukuliwa na madaktari hao ni muhimu katika kuwajengea uwezo Madaktari wazalendo, wauguzi na wafanyakazi wa Afya, kwa vile walipata fursa ya kufanya kazi pamoja na wataalamu wabobezi.Aidha, Dk. Mwinyi amefurahishwa kupata tathmin kutoka kwa wataalamu hao juu ya zoezi hilo lilivyokwenda kwa mafanikio makubwa.

Alieleza kuwa Serikali inaendelea kuzifanyia kazi changamoto mbali mbali zinazoikabili sekta ya Afya nchini na kusema inalenga kujenga Hospitali katika kila Wilaya zote na Mkoa ili kutoa huduma bora za Afya, na hivyo kuwahakikishia wataalamu hao kufanya kazi katika mazingira bora zaidi siku zijazo.Dk.Mwinyi alitoa shukran kwa juhudi na ukarimu mkubwa waliouonyesha wataalamu hao na kuwataka kuendeleza imani waliyonayo na kuja nchini miaka ijayo.Aidha, aliyashukuru Mashirika ya Pellex na Direct Aid Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali na kudhamini kambi hizo za utaoji tiba.

Nao kwa nyakati tofauti katika maelezo yao Madaktari hao; walimweleza Rais Dk. Mwinyi kufurahishwa kwao kwa kupata fursa ya kuja nchini kwa ajili ya kutoa huduma kwa ndugu zao wa Zanzibar.Walisema walifanyakazi wakiwa na imani ya kuwasaidia ndugu zao wa Zanzibar, huku wakibainisha furaha waliyonayo kutokana na ushirikiano na ukarimu ulionyeshwa na Wizara, Madaktari na wauguzi pamoja na wananchi waliowapatia huduma.

Madaktari hao wanaorejea nyumbani baada ya kumaliza jukumu hilo, waliahidi kuwa mabalozi na kutoa taarifa njema ya wananchi wa Zanzibar ili kuvutia Madaktari wengi zaidi kuja nchini siku zijazo ili kazi hiyo iwe endelevu.Sambamba na hilo waliahidi kutafuta njia bora ili kupanua wigo wa utoaji huduma nyenginezo, pamoja na kujenga mikakati na Serikali katika suala zima la upatikanaji wa vifaa vya tiba.

Nae, Mratibu wa Timu hiyo ya Madaktari katika Hospitali ya Wete, Dr. Hawala Saleh alisema jumla ya Operesheni 89 zilifanyika kwa mafanikio makubwa katika kambi hiyo ya siku saba katika Hospitali ya Wete, huku Operesheni 101 zikifanyika Hospitali ya Chakechake.Aliyataja miongoni mwa magonjwa yaliohusika na Operesheni hizo, kuwa ni Goita, Uvimbe katika kizazi, tenzi dume, koo, korodan isioshuka, mifupa, vijiwe katika figo, uvimbe kwa mama mzazi, uvimbe fuko la uzazi, mishipa pamoja na Ngiri.

Dr. Hawala alitumia fursa hiyo kumpongeza Mbunge wa Jimbo la Gando Salim Mussa Omar kwa juhudi kubwa aliyofanya kufanikisha kambi hiyo ya siku saba.Aidha Mbunge wa Jimbo la Gando (CCM)  Salim Mussa Omar aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya , Mashirika ya Pellix na Direct Aid Zanzibar pamoja na timu hiyo ya Madaktari wabobezi kwa kuwasaidia wananchi wa Zanzibar.

Alisema katika Jimbo la Uchaguzi analolitumikia la Gando (Wilaya Wete), jumla ya wagonjwa 21 walifanyiwa Operesheni mbali mbali, ambapo kiasi cha shilingi shilingi Milioni 84 ziliokolewa.