RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameishukuru Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa kuanza kushughulikia migogoro ya Ardhi inayolikabili Jeshi la Wananchi na Tanzania, hapa Zanzibar.

Dk. Mwinyi ametoa shukurani hizo Ikulu Zanzibar, alipozungumza na Waziri wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Innocent Bashungwa (MB) aliefika kwa ajili ya utambulisho.

Amesema kumekuwepo changamoto za migogoro ya ardhi inayolihusisha Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) na raia, hali iliosababishwa na ongezeko la makaazi ya wa wananchi katika maeneo ya migogoro.

Dk. Mwinyi alisema amefurahishwa na juhudi zilizoanza kuchukuliwa na Wizara hiyo katika kuitafutia ufumbuzi migogoro hiyo, huku akibainisha matumaini yake kuwa itamalizika vyema.

Aidha, alimhakikishia Waziri huyo kuwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itampa kila aina ya masharikiano ili kufanikisha majukumu ya kiulinzi.

Nae, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Innocent Bashungwa, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumkabidhi jukumu la kuiongoza Wizara hiyo, pamoja na kumshukuru Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi kwa kuweka misingi bora katika Wizara.

Waziri Bashungwa aliahidi kuendeleea kumsaidia Amiri Jeshi Mkuu katika ulinzi wa mipaka pamoja na kudumisha Muungano wa Tanzania.

Alisema Wizara yake iko mbioni kuitafutia ufumbuzi igogoro ya ardhi inayolikabili Jeshi la Wananchi wa Tanzania hapa Zanzibar