Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amekamilisha ziara yake katika Wilaya zote za Unguja na Pemba na kueleza jinsi alivyoridhika na hatua iliyofikiwa katika miradi mbali mbali ya maendeleo aliyoitembelea.Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo wakati akitoa majumuisho ya ziara yake katika Mkoa wa Kusini Pemba, ambapo leo anakamilisha ziara yake ya Mikoa yote mitano ya Unguja na Pemba iliyoanza Julai 16, 2022 hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Makonyo, Wawi Chake Chake katika Mkoa wa Kusini Pemba.
Alisema kwamba madhumuni ya ziara hiyo ni kupita katika Mikoa na Wilaya zikiwemo Wilaya ndogp na kukagua miradi ya maendeleo ikiwemo miradi ya UVIKO-19 pamoja na kufanya tathmini ya Ilani ya Uvhaguzi ya CCM na kusema kwamba lengo lake la kufanya ziara hiyo limetimia kwa mafanikio makubwa.“Namshukuru kwa kukamilisha ziara yangu katika Mmikoa yote”.Alisema kwamba miradi mbali mbali aliyoitembelea na mengine kuiwekea mawe ya msingi ameridhika nayo katika uendelezaji wake isipokwua mradi mmoja tu ambao haukufikia lengo lililokusudiwa.
Alitoa pongezi kwa Mkoa huo kwa kuendeleza amani na usalama katika MKoa huo na kueleza kwamba wananchi wanapaswa kupewa pongezi kubwa kwani hivi sasa wameungana na kuwa wamoja.
Alisema kuwa maendeleo yote yanayozungumzwa hayawezi kupatikana kama hakuna umoja, amani na usalama.
Rais Dk. Mwinyi alimpongeza Mkuu wa Mkoa na kusema kwamba yale maono yake ifike pahali Wakuu wa Mikoa kuonesha mipango na alichofanya ndicho kinachotakiwa na kuahidi kwamba Serikali itamsaidia.
Alieleza kwamba kama alivyoeleza katika Mikoa mengine, bado anataka hatua zaidi ziimarike katika Mabaraza ya Miji na atakapokuja tena mara ya pili anataka kuja kuzindua miradi ya Mabaraza ya Miji.
Aliyataka Mabaraza ya Miji kuwa na utaratibu mzuri wa kukusabya mapato na kuwataka kuwa na maono na kueleza namna Serikali itakavyoweka msaada katika kuwasaidia kwenye mikopo.
Alisema kwamba ujenzi wa “Mkoani Complex” ni kitu kizuri kilichobuniwa na Mkoa huo na kuwataka angalau asilimia 30 iyende kwenye maendeleo kwani tayari suala la madiwani limeshachukuliwa na serikali kuu.
Alisema kwamba miradi yote aliyoitembelea imefikia hatua nzuri na kuwapongeza wote waliosimamia miradi hiyo wakiwemo wafanyakazi katika ngazi za Wilaya, Mkoa, pamoja na wananchi.
Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba Wilaya ya Mkoani pekee ndio hawajapata hospitali ya Wilaya na hiyo ni kwa sababu Serikali imeamua kwa makusudi kuiboresha hospitali ya Abdalla Mzee.
Alieleza hatua zinazoendelea katika kuimboresha hospitali hiyo ambapo leo aliizindua sehemu ya kusafisha damu za wagonjwa wa figo yenye vitanda vitano ambayo ni ya kisasa na tayari ameanzisha safari ya kuimarisha hospitali hiyo ikiwa ni pamoja na kuweka Xray ya kisasa pamoja na gari inayotumia umeme kwa ajili ya wagonjwa .
Alisema kwamba hospitali ya Abdalla Mzee itawekewa vifaa na kuwataka Wizara ya Afya kuendelea kutoa vifaa pamoja na watoa huduma za afya.
Kwa upande wa sekta ya elimu, Rais Dk. Mwinyi aliitaka Wizara ya Elimu kutekeleza mpango mwengine wa kazi waliyoianza katika kuimarisha sekta hiyo kwani bado kuna mahitaji.
Kwa upande wa sekta ya maji alisema kuwa asilimia ya maji yanayopatikana hivi sasa ni 50 tu Unguja na Pemba hivyo, ni lazima kazi ya ziada ikafanywa na kueleza hatua zitakazochukuliwa na Serikali zikiwemo njia mbadala na kueleza kwamba tatizo la maji litaondolewa Unguja na Pemba.
Rais Dk. Mwinyi alimtaka Waziri wa Fedha kuhakikisha anamaliza suala zima la fidia kwani wananchi walio wengi ni masikini ili kazi zifanyike na wananchi wasinungunike.
Alitumia fursa hiyo kuipongeza benki ya CRDB kwa kufanya kazi nzuri ya dhamana waliyopewa na Serikali katika kutoa mikopo kwa Wajasiriamali.
Aliwashukuru wananchi waliokubali kutoa vipando vyao kwa ajili ya kujenga barabara na kuwashukuru kwa uzalendo wao na kueleza jinsi atakavyotafuta fedha za ziada ili zipate kuongezwa na barabara nyengine.
Akieleza kuhusu uchumi wa buluu, Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba bado hajarizika na ufugaji wa samaki, kaa na majongoo unaofanywa na kuitaka Wizara husika kuwasaidia wafugaji hao ikiwa ni pamoja na kuwatafutia vifaranga.
Alisisitiza haja ya kuongeza mikarafuu na kuitaka ZSTC kuja na mpango maalum wa kuongeza zao hilo ikiwa ni pamoja na kupanda mikarafuu mipya na kuongeza pembejeo katika zao hilo.
Rais Dk. Mwinyi alieleza miongoni mwa miradi mikubwa inayokusudiwa kuimarishwa na Serikali anayoiongoza huko kisiwani Pemba ikiwa ni pamoja na ujenzi wa uwanja wa ndege wa Pemba ambao utasaidia kuifungua Pemba ambapo ndege zote kubwa zitaweza kutua kisiwani humo.
Alizieleza hatua nyengine zitakazochukuliwa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa bandari ya Pemba na kueleza hamu yake ya kuona mradi mkubwa wa bandari unaimarishwa badala ya uliopo hii sasa na kuona meli zinazotoka Dubai na sehemu nyenginezo zinafunga gati katika bandari hiyo.
Alieleza hatua ambazo zinazochukuliwa katika ujenzi wa barabara kuu zikiwemo barabara ya Cheke- Mkoani na Chake- Wete pamoja na kuweka eneo maalum la viwanda katika eneo la Chamanangwe kisiwani Pemba.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba baada ya ziara hiyo kilichobaki ni kazi na kuhakikisha miradi yote aliyoahidiwa inamaliza kwa wakati.