RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amekutana na Mkuu mpya wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Gen. Jackob John Nkunda aliefika Ikulu kujitambulisha na kumpongeza kwa dhati kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo.

Dk. Mwinyi amemuomba Mwenyezi Mungu kumfanyia wepesi kiongozi huyo katika utekelezaji wa kazi zake, huku akibainisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania kupata Kiongozi sahihi mwenye uwezo wa kulisogeza mbele kutoka hapo lilipo.

Alimuahidi mashirikiano kiongozi huyo, hususan katika utatuzi wa changamoto zitakazojitokeza katika utendaji wake, huku akionyesha imani kubwa kwake   kwa kuwa na weledi na uwezo mkubwa.

Nae, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Gen. Jackob John Nkunda alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kumpandisha cheo na hatimae kumteua kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini, sambamba na Uteuzi wa Mnadhimu mkuu wa JWTZ Lt. Gen Salum Haji Othman .

Aidha, akatumia fursa hiyo kumpongeza mtangulizi wake Gen. Mabeyo kwa kazi kubwa aliyofanya ya kuliimarisha Jeshi hilo.