RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amempongeza Mwekezaji wa Hoteli ya RUI JAMBO kwa imani kubwa alionyesha na kufanikisha Uwekezaji wa   mradi mkubwa wa Hoteli ya Kitalii.Dk. Mwinyi ametoa pongezi hizo katika uzinduzi wa Hoteli hiyo, hafla iliofanyika Nungwi Mkoa Kaskazini Unguja, ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kutembelea miradi mbali mbali katika Mikoa ya Unguja na Pemba, ikiwemo ile inayoendelezwa kupitia fedha za Ahueni ya Uviko – 19.

Amesema hatua ya Mwekezaji huyo kuwekeza Hoteli kubwa ya Nyota Nne hapa nchini, imewajengea imani Wawekezaji wengine kuja kuwekeza nchini katika miradi mikubwa.

Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuipongeza Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) kwa utendaji kazi mzuri na kuitaka taasisi hiyo kuendelea kuboresha mazingiya Uwekezaji ili kuvutia Wawekezaji wengi zaidi.

Alisema kukamilika kwa Hoteli hiyo kutawawezesha Wazanzibari kunufaika ipasavyo na ajira na kabainisha kuwa Watanzania wapatao 350 tayari wameajiriwa hotelini hapo na kueleeza kuwa wakati ujenzi ukiendelea kulikuwa na wananchi wengi waliopata ajira za muda, ikiwemo mafundi.

Aidha, alimpongeza Mwekezaji huyo kwa kutoa ajira kwa wananchi sambamba na kununua bidhaa mbali mbali kwa ajili ya matumizi ya Hoteli kutoka hapa hapa nchini,ikiwemo bidhaa za kilimo pamoja na uvuvi na hivyo kutoa fursa kwa wananchi hao ya kujiongezea kipato.Dk. Mwinyi   alieleza kuwa Hoteli hiyo imekuwa ikiitangaza Zanzibar kimataifa, hatua itakayochochea ujio wa watalii wengi hapa nchini.

Katika hatua nyengine, Dk. Mwinyi alisema Serikali imejidhatiti kuja na miradi mikubwa wa maji ya uhakika katika maeneo hayo, ili kuwawezesha wananchi na Wawekezaji kupata huduma hiyo kwa uhakika.Katika utekelezaji wa jambo hilo, Dk. Mwinyi aliwataka wananchi kuwa walinzi wa miundombinu ya maji, huku akibainisha kuwepo wananchi wanaoharibu kwa makusudi miundombinu hiyo ili kupata fursa ya kupeleka maji katika Hoteli kwa njia ya magari na kujiingizia kipato.

Aidha Dk. Mwinyi alisema Serikali ina mpango wa kuleta vifaa vipya na vya kisasa vya upakuzi wa mizigo Bandarini, ikiwa ni juhudi za kuharakisha kazi za kupakua mizigo, ikiwemo ya Wawekezaji.Alitumia fursa hiyo kuwatia moyo wananchi juu ya kuanza kwa ujenzi wa Bandari ya Mangapwani hivi karibuni na kusema ‘ hivi karibuni Serikali itasaini mkataba ujenzi wa Bandari ya Mangapwani na kutoa fursa za ajira kwa wananchi, hususan wa Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Aidha, aliwataka Vijana wanaotembeza wageni ‘Beach Boys’ kujiandaa kwenda katika maeneo maalum yanayotayarishwa kwa ajili ya uuzaji wa bidhaa mbali mbali z aujasiriamali, ikiwa ni hatua ya kuondoa bughudha kwa Watalii.

Nae, Waziri wa Uwezeshaji Mudrik Ramadhan Soraga alisema katika kipindi cha Awamu ya nane, chini ya Uongozi wa Dk. Mwinyi, nchi imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuvutia Wawekezaji, kiasi ambacho wale waliokuwa wamekata tamaa wameanza kuja kuwekeza na akatumia fursa hiyo kuipongeza ZIPA kwa utendaji uliotukuka.Aidha, Waziri wa Utali na Mambo ya Kale Simai Mohamed Said alimtaka kila Mzanzibari kuwa Balozi katika uimarishaji wa sekta hiyo ili kutangaza na kuvutia watalii, kwa lengo la kukuza Uchumi wa Taifa.

Vile vile Mwekezaji wa Hoteli hiyo Carlos alisema Hoteli hiyo ina azma ya kuwafanya wafanyakazi, wana jamii na wananchi wanaotoa huduma mbali mbali Katika hoteli hiyo kufurahia na uwepo wake.

Hoteli ya RUI Jambo hadi kufikia sasa ina jumla ya Vyumba 461 na pale itakapokamilika itaweza kuwa na vyumba 1000, ikiwa tayari imetumia Dola Milioni 61 hadi sasa na kutoa ajira 368.