RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi amesema amani, umoja na mshikamano ndio siri ya mafanikio yaliyopatikana ndani ya kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Serikali ya awamu ya nane.Alieleza kufunguliwa kwa miradi ya Maendeleo ya miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar kunatokana na kuwepo kwa mapenzi makubwa ya wananchi kwa viongozi wao jambo alilolisisitiza kuendelezwa ili Maendeleo zaidi yaongezeke kama ilivyo azma ya Serikali anayoiongoza.

Dk, Mwinyi alisema hayo kwenye ufunguzi wa Hospital ya Wilaya, Micheweni kisiwani Pemba ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Alieleza ufunguzi wa miradi kama hiyo ni kuyaenzi na kuyathamini Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kujenga Hospital katika ngazi mbalimbali ikiwemo za Wilaya kama hiyo, Mikoa hadi Taifa.

Alisema ndani ya miaka mitano ya Uongozi wake, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatarajia kukamilisha haspitali zenye ubora katika mikoa yote ambazo zitatoa huduma bora za Afya na hazitomfanya mwananchi kusafiri nje ya nchi kufuata matibabu.Dk, Mwinyi aliwataka watoa huduma za Afya wakiwemo Madaktari, Wauguzi na wahudumu wa afya kuwa na lugha nzuri kwa wagonjwa wanaowahudumia kwani lugha nzuri nazo ni tiba.

Naye Waziri wa Afya, Nassor Ahmed Mazrui aliahidi kuwa Wizara hiyo itaendelea kusimamia na kutekeleza maagizo yote ya Rais kuhakikisha inakuwa na mageuzi kwenye utoaji wa huduma bora za matibabu ili wananchi wanapate huduma nzuri zaidi.Hospital ya Wilaya ya Micheweni Pemba, ilikadiriwa kutumia zaidi ya shilingi billion 6 hadi kufunguliwa kwake na tayari imeshatumia zaidi ya shilingi Billion 5.Hospitali hiyo itatoa huduma mbalimbali muhimu za matibabu. zikiwemo chumba cha ICU, dharura, Vitanda vya kujifungulia na huduma za ICT.