Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Hayati Dr, Mwelecele Ntuli Malecela (Dr. Mwele) ni mwanataaluma aliejitolea kwa dhati kulipigania Taifa la Tanzania, ili kufikia lengo la kuondokana na magonjwa yasiopewa kipaumbele.Dk. Mwinyi amesema hayo katika salamu alizotoa kwa waombolezaji wakati wa kuaga mwili wa Hayati Dr. Mwelecele Ntuli Malecela, hafla iliofanyika katika viwanja vya Karimjeee Jijini Dar es Salaam.
Amesema katika kipindi cha miaka 30 akiwa mtumishi wa Serikali katika taasisi ya Utafiti wa magonjwa yasiopewa kipaumbe(NIMRY), Hayati Dr. Mwele alifanya kazi kubwa ya kuanisha Programu ili kutokomeza magonjwa yasiopewa kipaumbele, ikiwemo Matende na mabusha, minyooo ya Tumbo, kichocho, Trachoma pamoja na Usubi.
Alisema Hayati Dr. Mwele alifanya kazi kubwa ya kulitumikia Taifa , hivyo akawataka Watanzania kujitathmin endapo utumishi wao utafikia kiwango kilichoachwa na hayti Dr. Mwele.
Akizungumza kwa niaba yake na kwa niaba ya Familia ya Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mwinyi amesema kifo cha Hayati Dr. Mwele kimemgusa kila Mtanzania, kwani alikuwa mtu wa watu alietumia muda wake wote kuwatumikia wananchi.
Akinukuu kauli za viongozi wa Dini, aliwataka Watanzania kujifunza kutoka kwa yale yaliofanywa na Dk. Mwele, kwa kutambua kuwa kutokana na vifo hupatikana mawaidha pamoja na hadithi njema.
Aidha, alisema ni wajibu wa wananchi kumuombea Dua hayati Dr. Mwele, pamoja na kuiombea familia yake ustahamilivu katika kipindi hiki kigumu.
Nae, Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa katika salamu zake alisema kifo cha Hayati Dr. Mwele kimeleta huzuni kubwa kwa kuzingatia mchango wake mkubwa aliotoa katika kulitumikia taifa.
Aidha, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Tulia Akson aliwataka Watanzania kuendeleza mambo mema yalioachwa na hayati Dr. Mwele, kwa maslahi ya Taifa na watu wake, huku akiwatakia pole wafiwa.
Katika hatua nyengine, Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Joseiph Sinde Warioba alisema Hayati Dr. Mwele alikuwa mwanamke anaejiamini sana, kiasi ambacho katika mwaka 1995 alifikia uamuzi wa kuchukua fomu kugombea kiti cha Urais.
Dr. Mwelecele Ntuli Malecela aliekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) anaeshughulikia magonjwa yasiopewa kipaumbele alizaliwa mnamo mwaka 1963 na kufariki dunia mapema wiki Geneva Switzerland, wakati akiwa nchini alikuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu nchini Tanzania (NIMR)