RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi   Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema ili Taifa liweze kupata mafanikio, kunahitajika uwepo wa vipaumbele na shabaha zinazoweza kupimika, sambamba na mipango ilio makini na ufuatiliaji.Dk. Mwinyi amesema hayo katika Uzinduzi wa Taasisi ya Afisi ya Rais ya Ufuatiliaji na Usimamizi wa Utendaji Serikalini ( PDB), hafla iliofanyika katika Viwanja vya Ikulu Zanzibar.

Amesema mafanikio yanahitaji kuwepo kwa vipaumbele, mipango makini ya ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kuweza kutatua matatizo yanayojitokeza na kuepuka ucheleweshaji.alisemasema jukumu kubwa la PDB ni kuhakikisha kunakuwepo utekelezaji wa vipaumbele vilivyoainishwa kwa wakati unaofaa.

Alisema kwa kuanzia utekelezaji wa vipaumbele hivyo utahusisha sekta nne za miundombinu,Utalii, Maendeleo ya Kijamii pamoja na Uchumi wa Buluu.Dk. Mwinyi alieleza kuwa PDB ni kitengo maalum kilioko chini ya Ofisi yake, kinachoundwa na timu ya wataalamu walioajiriwa kwa utaratibu wa ushindani na uwazi.

Alisema taasisi hiyo itaondoa vikwazo, kubaini uhaba wa rasilimali na masuala mengine yanayoweza kuchelewesha maendeleo, ili kufanikisha lengo la utekelezaji wa ahadi zake kwa Wananchi.Aliwataka Viongozi na watendaji Seriklai kubadilisha na kuharakisha njia za kufanyia kazi kwa kuondokana utendaji na mazoeya .

Aidha, alisema ili kufikia mafanikio, Taifa linapaswa kujifunza kutoka kwa wengine na kukubali usaidizi kutoka kwa wahisani na marafiki, kama vile Taasisi ya Tony Blair (TBI) na UNDP, huku mkazo ukiwekwa katika kuwajengea uwezo watendaji.Alitoa wito kwa wananchi wote wa Zanzibar kushirikiana na taasisi hiyo, huku kila mmoja akiwajibika kwa nafasi yake.

Nae, Waziri wa Nchi (OR) Ikulu, Jamal Kassimu Ali alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyektii wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi kwa kuona haja na umuhimu wa kuanzisha taasisi hiyo na kubainisha imani aliyonayo kuwa itamsaidia kukamilisha dhamira yake katika kipindi cha Uongozi wake.Aidha, alitoa pongezi kwaTaasisi za Tony Blair, Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) pamoja na timu nzima ya Watendaji wa PDB kwa kufanikisha uanzishaji wa taasisi hiyo.

Mapema, Mwakilishi wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Christine Musisi aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kazi kubwa ya kuhakikisha inakuwa karibu na wananchi kwa kuweka mazingira mazuri na sekta zote na kufanyakazi kwa ufanisi.Alisema ili kufanikisha dhamira ya kutoa huduma bora kwa wananchi ni lazima kuwepo vipaumbele na akatumia fursa hiyo kuipongeza Serikali kwa kuanzisha taasisi hiyo.

Alieleza kuwa PDB itakuwa daraja la kuunganisha mahitaji ya Serikali, sekta binafsi pamoja na wananchi katika utekelezaji wa malengo ya Taifa na yale ya Kimataifa. Sambamba na hayo alisema UNDP itaendelea kushirikiana na Serikali katika utatuzi wa changamoto mbali mbali.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Viongozi mbali mbali wa Kitaifana Kimataifa, wakiwemo Mawaziri, Mabalozi, Washirka wa Maendeleo, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama pamoja na Viongozi wa Dini.