Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Kiswahili kimekuwa ni daraja muhimu la kuimarisha uhusiano na utengamano katika maendeleo ya uchumi, biashara, siasa na diplomasia katika ukanda wa Afrika ya Mashariki, Bara la Afrika na Dunia nzima.Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo wakati akifunga Kongamano la Pili la Idhaa za Kiswahili Duniani lililofanyika kwa muda wa siku tano, huko katika ukumbi wa Mikutano wa ICC, Jijini Arusha ambao umeandaliwa na BAKITA na BAKIZA na kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 200 lenye kauli mbiu isemayo “Tasnia ya Habari kwa Maendeleo ya Kiswahili Duniani”.
Alisema kuwa hali hiyo imechangiwa na jitihada za viongozi wakuu waliopo na waliotangulia katika kuikuza lugha ya Kiswahili ambapo pia, jitihada za Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan zinaonekana katika kukindeleza Kiswahili kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake Marehemu Dk. John Pombe Magufuli ambao wote wameunga jitihada za Viongozi wa Tanzania waliotangulia katika kuikuza na kuindeleza lugha hiyo.Rais Dk. Mwinyi alileza kuwa kutokana na jitihada hizo, Kiswahili kimeendelea kupata mafanikio kwa kuwa lugha ya kwanza ya Kiafrika kuwekewa siku maalumu ambapo pia, lugha hii imeweza kupitishwa kuwa miongoni mwa lugha za kazi katika Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SACD) pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Alieleza kuwa sababu nyengine inayochangia kuongezeka kwa wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili ni kutokana na mchango na kuongezeka kwa idadi ya vituo vya Redio vinavyotangaza kwa lugha ya Kiswahili na kutolea mfano idadi ya Redio zinazotoa matangazo kwa lugha hiyo hapa Tanzania hivi sasa imefikia 183.Aliongeza kuwa licha ya ongezeko la idhaa zinazotangaza kwa lugha ya Kiswahili hapa Tanzania, vile vile, kuna ongezeko kubwa la idhaa za nje ya nchi zinazotangaza kwa lugha hii adhimu ya Kiswahili ambapo, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2021, idadi ya idhaa za nje zinazotangaza kwa lugha ya Kiswahili ni zaidi ya 39.
Alieleza kuwa idadi ya vituo vya Televisheni nchini vinavyotoa matangazo yake kwa lugha ya Kiswahili pia imekua ikiongezeka kila mara ambapo hadi sasa imefikia zaidi ya vituo 45 ambapo Magazeti nayo yameongezeka kutoka sita tu yaliyokuwepo nchini kabla ya Uhuru na hivi sasa kufikia 283.Alisema kuwa kuna mchango muhimu wa kuongeza wazungumiaji wa Kiswahili kupitia usomaji wa maandiko ya vitabu na makala kadhaa za Isimu na Fasihi ambapo Kamusi za Kiswahili na Majarida ya taaluma mbali mbali yameweza kuandaliwa katika kipindi cha baada ya Uhuru na kusaidia sana maendeleo na ukuaji wa Kiswahili hapa Tanzania pamoja na nchi za nje zinazojifunza lugha hii.
“Mafanikio ya kukua kwa matumizi ya lugha ya Kiswahili hivi sasa tunayashuhudia pia kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA). tayari Kampuni ya Microsoft zimetayarisha programu za Kompyuta kwa ajili ya lugha za Kiafrika kikiwemo Kiswahili”,alisema Dk. Mwinyi.Hivyo,Rais Dk.Mwinyi alisema kuwa watumiaji wa Programu za Microsoft wana uwezo wa kupata nakala za Microsoft zote ambapo hiyo ni hatua kubwa ya maendeleo ya lugha ya Kiswahili kwenye TEHAMA.
Alieleza kuwa, pamoja na mafanikio hayo makubwa zimejitokeza changamoto kadhaa zikiwemo kuibuka kwa misamiati mipya na utohoaji usiozingatia taratibu za vyombo vya kusanifu lugha (BAKITA na BAKIZA) kwa Tanzania,kunako sababisha kuwepo kwa mkanganyiko ambao huwakwaza zaidi wazungumzaji wapya wa Kiswahili.
Hivyo, alieleza kwamba mafanikio ya kongamano hilo ni pamoja na kutoka na maazimio na mikakati ya kuweza kuwa na matumizi sawa ya msamiati wa lugha ya Kiswahili katika vyombo vyote vya habari vinavyotumia lugha ya Kiswahili.
Aliongeza kuwa vyombo vya habari vina mchango ama wa kutengeneza au kuharibu zaidi na kuvitaka kuwa tayari kujifunza kutoka kwa wataalamu na taasisi zinazosimamia maendeleo na ukuaji wa lugha ya Kiswahili ambao ni washiriki muhimu wa kongamano hilo.Alisema kuwa Serikali itaendelea kuziwezesha taasisi za BAKITA na BAKIZA ili zimudu kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ikiwemo kufanya tafiti mbali mbali za Kiswahili, na kuzijengea uwezo zaidi wa kutoa mafunzo na kuwasaidia wadau mbali mbali wa Kiswahili.
Kwa upande wa Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane, itaendeleza jitihada zilizoanzishwa na viongozi wa Awamu zilizotangulia katika kuimarisha lugha ya Kiswahili hasa kwa kuzingatia kuwa Zanzibar ni kitovu cha lugha hiyo.Kadhalika, alisema kwamba Serikali itaimarisha mafunzo ya ufundishaji wa Kiswahili kwa Wageni katika iliyokuwa Taasisi ya Kiswahili na Lugha ya Kigeni (TAKILUKI) iliopo chini ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kwa kuwapatia vifaa na nyenzo za kisasa kwa lengo la kuimarisha na kurudisha hadhi na uwezo wa kituo hicho ambao kwa miaka ya karibuni umepungua.
Zaidi ya hayo, Rais Dk. Mwinyi aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuandaa Kongamano la kila mwaka la Kiswahili la Kimataifa ambalo tayari limeshafanyika mara tano (5) na kuhudhuriwa na Wataalamu wabobezi na wapya wa lugha ya Kiswahili kutoka sehemu mbali mbali Duniani.Aidha, Rais Dk. Mwinyi alitoa mwaliko kwa washiriki hao kwamba Kongamano lijalo lifanyike Zanzibar na kuahidi kwamba Serikali itatoa ushirikiano wa kutosha.
Nae Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Omar Mchengerwa alipongeza juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi za kukiimarisha Kiswahili huku akiomba kuanzishwa kwa vituo vya utamaduni na sanaa katika Balozi zote za Tanzania duniani.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita kwa upande wake alisema kuwa kumekuwa na Mashirikiano makubwa kati ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Wizara anayoiongoza na kuahidi kuimarisha uhusiano na ushirikiano huo ili Kishwahili kizidi kuimarika ndani na nje ya nchi.
Nao wawakilishi wa Idhaa za Redio za Kiswahili za nje na ndani ya nchi walipata fursa ya kueleza jinsi vituo vyao vinavyofanya kazi sanjari na mafanikio waliyoyapata huku wakitoa pongezi kwa kuandaliwa na kualikwa katika Kongamano hilo ambapo pia, viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walipata fursa ya kueleza jinsi lugha hiyo wanavyoiimarisha.Katika ufungaji wa Kongamano hilo, Rais Dk. Mwinyi alitunukiwa tunzo maalum ya kuthamini mchango wake katika kukikuza Kiswahili ambapo pia, alipata fursa ya kuzindua program ya ufundishaji wa Kiswahili Mtandaoni pamoja na kutoa vyeti kwa washiriki na wadhamini mbali mbali wa Kongamano hilo.
Mapema, Rais Dk. Mwinyi alitembelea eneo maalum lililotengwa katika ukumbi huo kwa ajili ya maonyesho ya vitabu mbali mbali vikiwemo vile vya Kiswahili sanifu.