Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa kwa vile maji ni uhai lazima Serikali iongeze kasi ya upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi kwa kuendeleza na kuanzisha miradi mipya ya maji safi na salama.Rais Dk.Mwinyi aliyasema hayo leo katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la Mradi mkubwa wa Uhuishaji na Uimarishaji wa Mfumo wa Maji Safi na Salama, huko Kwarara Kidutani, Wilaya ya Magharibi ‘B’, Mkoa wa Mjini Magharibi ikiwa pia, ni kipindi ambacho Dunia inaadhimisha Wiki ya Maji.

Katika hotuba yake Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo uliowekwa jiwe la msingi ni katika kuyafikia malengo hayo huku akisisitiza kwamba hatua hiyo ni ndani ya miaka miwili tu na hana shaka ndani ya miaka mitano ijayo tatizo la maji litamalizika.Alisema kuwa takwimu zinaonesha kwamba hali ya upatikanaji wa maji nchini hivi sasa ni wastani wa asilimia 55 hadi kufikia mwaka huu wa 2022 na kueleza kwamba kukamilika kwa mradi huo asilimia zitaongezeka na kufikia 76 huku juhudi zaidi zikichukuliwa katika kuhakikisha wananchi wote wanapata maji safi na salama.

Rais Dk. Mwinyi alitoa wito wa Wizara husika pamoja na Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kufanya kazi na kuwa wepesi wa kutatua changamoto za huduma hiyo zinazowakumba wananchi.Alisisiatiza kwamba jukumu la ulinzi la miundombinu ya maji ni la watu wote na kueleza kwamba wananchi wanajukumu la kuilinda miundombinu hiyo na wasiwaruhusu watu wachache kuiharibu.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa upatikanaji wa huduma za maji safi na salama katika maeneo yote ya Unguja na Pemba ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.Hivyo, aliongeza kuwa jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika upatikanaji wa huduma za maji safi na salama ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2020-2025, Mipango mikuu ya maendeleo na ahadi zilizotolewa katika kipindi cha kampeni.

“Leo tarehe 21, Machi 2022 tupo hapa Kwarara Mkoa wa Mjini Magharibi, kufungua ukurasa mwengine wa maendeleo ya sekta ya maji kwa kuweka jiwe la msingi la mradi mkubwa wa kuimarisha upatikanaji wa huduma za maji katika maeneo mbali mbali ambapo huduma hii haipatikani kabisa”, alisema Dk. Mwinyi.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa mradi huo utanufaisha zaidi maeneo ambayo kwa sasa yanaonekana kukua kwa haraka kutokana na wananchi wengi kujenga makaazi yao mapya na kuhamia maeneo hayo ya Wilaya ya Magharibi ‘A’ na Magharibi ‘B’ pamoja na maeneo ya mpakani mwa Mkoa wa Mjini na Magharibi na Mkoa wa Kusini Unguja yakiwemo Tunguu, Jumbi na Ubago.Alisema kuwa maadhinisho hayo ambayo yanakwenda na ujumbe wa kauli mbiu isemayo “Rasilimali za maji chini ya ardhi ni nyenzo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi” na kusisitiza kuwa na mipango mbadala na mikakati itakayowezesha kukabiliana na changamoto za aina tabianchi.

Alieleza kwamba hali ya tabianchi ndio inayopelekea uwezo wa uzalishaji wa maji katika vyanzo vilivyopo kupungua kama inavyoshuhudiwa katika vyanzo vya Mwanyanya na Mtopepo.Alisisitiza kwamba katika hali kama hiyo ni lazima wananchi waendelee kupewa elimu ya kuvilinda na kuvitunza vyanzo vya maji kwa kuepuka ujenzi karibu na vyanzo hivyo na kuacha tabia ya ukataji wa miti na misitu pale vilipo.

Rais Dk. Mwinyi alitoa wito kwa wananchi kuona haja ya kulipia maji ili huduma za maji ziwe endelevu na kuwataka ZAWA kuendelea kuweka mita za maji pamoja na kuhakikisha wanaotakiwa kulipa maji ni wale wanaoipata huduma hiyo na siyo kwa kila mwenye mfereji (bomba) ndani hata ikiwa maji hapati.

Nae Waziri wa Maji, Nishati na Madini Shaib Hassan Kaduara alitoa pongezi kwa Rais Dk. Mwinyi hukua akiahidi kwamba Wizara yake itaendelea kusimamia miradi yote ya maji ili kufikia lengo lililokusudiwa.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa alieleza jinsi wananchi wa Mkoa huo pamoja na Mikoa jirani watakavyofaidika na mradi huo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi-ZAWA Meja Jenerali Issa Nassor alieleza jinsi mradi huo pamoja na miradi mengine ya maji itakavyotekelezwa na kuwataka wananchi kuwa walinzi wa miundombinu ya miradi yote ya maji.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa ZAWA Dk. Salha Mohammed alisema kuwa Mradi huo unatekelezwa kwa mashirikiano ya pamoja kati ya Benki ya Exim ya India pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.Alisema kuwa Mradi wote hadi kukamilika kwake utagharimu jumla ya Dola za Marekani Milioni 92.18 ambazo zimetolewa na Serikali ya India kupitia Benki ya Exim ya India kwa njia ya mkopo wa masharti nafuu kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Aliongeza kuwa hadi hivi sasa wastani wa TZS 702,626,900 zimetolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwa ni sehemu ya mchango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ajili ya gharama za malipo ya fidia kwa mali na mazao ya wananchi yaliyoathirika na ujenzi wa mradi huo pamoja na gharama za uendeshaji wa mradi.Sambamba na hayo, alisema kuwa mradi huo umegawika sehemu tatu kwa utekelezaji wake ambapo sehemu ya kwanza itatekelezwa na Kampuni ya Megha Engineering Limited kutoka India na sehemu ya pili itatekelezwa na Kampuni ya Afcons and Vijeta-VJ ya India na sehemu ya tatu itatekelezwa na Kampuni ya Larsen& Toubro (L&T) Limited nayo ya India.

Nae Mwakilishi wa Jimbo hilo Ali Ameir Mrembo kwa niaba ya wananchi wa Jimbo hilo alitoa pongezi na shukurani kwa Rais Dk. Mwinyi kwa kuwapelekea huduma hiyo muhimu katika kipindi kifupi alichokaa madarakani.