RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali haina tatizo na kikundi cha Wajasiriamali kuongezewa kiwango zaidi cha mkopo, baada ya kumaliza malipo ya mkopo wa awali.Dk. Mwinyi amesema hayo katika Viwanja vya Skuli ya Kiembe samaki wakati alipoonana na kuzungumza na Vikundi vya Wajasiariamali mbali mbali waliopata mikopo kupitia Fedha za Uviko -19, ikiwa ni muendelezo wa ziara yake katika Wilaya ya Magharibi ‘B’  Unguja.

Amesema Serikali haina taizo na vikundi vya wajasiariamali vinavyokopesheka pale wanapohitaji kuongezewa kiwango zaidi cha mkopo baada ya kukamilisha malipo ya mkopo awali.

Alizitaka taasisi zinazosimamaia utoaji wa mikopo hiyo kuendelea kutoa taaluma kwa wajasiriamali ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanaweza kukopeshwa.

Dk. Mwinyi aliwashukuru wajasiriamali wote walioanza kulipa mikopo yao, sambambana kukipongeza kikundi cha Ujasiriamali cha Usafi kutoka eneo la Michungwani kwa kufanikiwa kupata mkopo wa gari la kuzolea taka, ikiwa ni mafanikio makubwa kwao, kwa vile walianza kazi hizo kwa kutumia ‘wheelbaro’.

Katika hafla hiyo Dk. Mwinyi alikabidhi Gari la kuzolea taka kwa kikundi hicho.

Katika hatua nyengine Dk. Mwinyi aliweka Jiwe la Msingi la Skuli ya Kimataifa ya ‘ZAN COASTAL ACADEMY’ iliopo Nyamanzi ambayo inafuata Mitaala ya Cambridge na kumpongeza Mwekezaji wa skuli hiyo kwa kuona umuhimu wa elimu, eneo ambalo lina manufaa makubwa kwa taifa.

Alisema taifa lolote lenye watoto walioelimika ni wazi kuwa litapiga hatua kubwa za amendeleo, hivyo akaahidi Serikali kuendelea kushirikiana na Sekta binafsi, kwa kutambua peke yake haiwezi kufanya kila jambo.

Alisema Serikali itashirikiana na wawekezaji wa eneo hilo na kuchukua hatua ya kuzitafutia ufumbuzi changamorto ziliopo, ikiwemo ile ya miundo mbinu ya barabara,na kusema tayari kuna mradi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha Lami kutoka Fumba hadi Kisauni.

“Tunatambua umuhimu wa kuweka miundo mbinu katika maeneo hayo”, alisema.

Alirudia kauli yake ya kuwataka wananchi waishio vijiji jirani na maeneo hayo ya Uwekezaji kuacha uvamizi wa maeneo kwa shughuli za ujenzi na kubainisha kuwa maeneo hayo ni muhimu kwa Uchumi wa Taifa.

Aidha, Rais Dk. Hussein Mwinyi alitembeela Mradi wa Uhuishaji na Uimarishaji wa Maji safi katika eneo la Dimani na kuitaka Wizara ya Maji, Nishati na Madini pamoja na Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA)  kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa mujibu wa Mikataba ilivyo.

Pia, aliwataka wananchi kuondokana na utamaduni wa kujenga pembezoni mwa barabara, kwani hatua hiyo huitatiza Serikali pale inapotaka kuendeleza miradi mbali mbali, ikiwemo ya maji safi na salama .

Alisema kuna nyakati Serikali hulazimika kutumia fedha nyingi kwa ajili ya kulipa fidia ya majengo na vipando vya wananchi vilivyoko pembezoni mwa barabara zaidi ya gharama za Mradi husika, hatua aliyosema baadhi ya nyakati Serikali hulazimika kuacha kutekeleza miradi hiyo.

Vile vile, Dk. Mwinyi alipata fursa ya kutembelea majengo ya Skuli iliofanyiwa matengenezo makubwa katika eneo la Bweleo ambapo kabla ilikuwa inamilikiwa na Mwekezaji kutoka nchini Korea na hatiame kununuliwa na Serikali na akaitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kufikiria matumizi mazuri ya majengo ya skuli hiyo.

Aidha, aktika ziara hiyo Dk. Mwinyi alitembelea eneo la Uwekezaji linalomilikiwa na Wawekezaji wazalendo la AFRICAB liliopo eneo la Fumba linaloshughulika na Uwekezaji wa Hoteli pamoja na nyumba za Kukodisha.

Ziara hiyo itaendlea tena kesho, ambapo Dk. Mwinyi atapata fursa ya kutemebela miradi mbali mbali ya maendeleo katika Wilaya Mjini Unguja.