Media » News and Events

Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali ina wajibu wa kutenga bajeti ya kuwawezesha watumishi wake hususan wa kada ya watunza kumbukumbu

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali ina wajibu wa kutenga bajeti ya kuwawezesha watumishi wake hususan wa kada ya watunza kumbukumbu.Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo Ikulu, Zanzibar alipozungumza na uongozi wa Chama Cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania, (TRAMPA) uliofika kujitambulisha.

Alisema bado Serikali ina wajibu wa kuwapeleka masomoni na kuwaongezea uwezo watunza kumbukumbu na watumishi wengine wa umma ili kuwajenga uweledi katika kukidhi haja ya taaluma zao.Alisema, chama cha TRAMPA ni mfano wa kuigwa na taasisi nyingine nchini ambacho kimejikita kwenye weledi wa hali ya juu wa kuwainua wanachama wake kitaaluma na ufanisi.

Rais Dk. Mwinyi, alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa kuuleta mkutano mkubwa wa chama cha TRAMPA kwenye visiwa vya Zanzibar, nakueleza kuwa mbali na kufanikisha malengo ya mkutano huo, pia umeakisi dhima ya utalii wa ndani.Dk. Mwinyi alieleza asilimia 30 ya uchumi wa Zanzibar unatokana na sekta ya Utalii, hivyo Mkutano wa TRAMPA uliinufaisha sana Zanzibar kiuchumi na biashara hasa kwa sekta za umma, binafsi na wananchi wakawaida.

Akizungumzia masuala ya Utalii kwa wanachama hao wa TAMPA ambao walimzawadia Rais Dk. Mwinyi zawadi ya sanamu ya mnyama wa Twiga ambae anasadifu utalii wa Wanyama uliopo nchini kupitia rasilimali za misitu na mbuga za Wanyama ambavyo ni vivutio vikubwa kwa wageni na watalii wanaofika nchini.Dk. Mwinyi alieleza, Zanzibar na Tanzania Bara kuna ushirikiano mkubwa katika kuitangaza na kuishajihisha sekta ya utalii hususani wageni na watalii wanaobahatika kuitembelea Tanzania, kwa pande zote mbili za Muungano hushajihishwa kutembelea vivutio vya utalii kwa sehemu yoyote ile wanayofikia.

“Hapa Zanzibar tuna jambo moja ambalo tunalitumia vizuri, kwamba wageni wanaotaka kwenda kwenye mbuga, kule Tanzanaia Bara kwa uwindaji au iwe safari tu za kuangalia Wanyama, aidha wanaanza kule lakini kisha lazima waje Zanzibar na wakianza huku lazima waende Bara” Alifafanua Dk. Mwinyi.Alieleza, Tanzania imeweka utaratibu mzuri wa kuendelea kuutangaza utalii kwa nguvu zote, nakueleza kuwa kitu ambacho kimeunganisha na kuendelea kuweka nguvu zaidi ili watalii wote wanaokuja Tanzania japo kwa siku chache basi wapate nafasi ya kuja Zanzibar na wanaoanzia Zanzibar pia waende Bara.

Pia, Rais Dk. Mwinyi alieleza faida za mkutano wa TRAMPA visiwani hapa, kwamba uliwanufaisha wazawa wengi kuanzia wafanyabiashara wenye maduka, vyakula, hoteli, nyumba za wageni hata sekta ya usafirishaji wakiwemo madereva taxi, bodaboda, daladala na wafanyabiasahara wengine.Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mwenyekiti wa TRAMPA, Devota George Mrope aliiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoa ushirikiano kwa kuwaruhusu watunza kumbukumbu wake kuhudhurra mafunzo mbalimbali yatakayoandaliwa na chama hicho popote, ndani na nje ya Zanzibar ili kuwaongezea weledi na uwezo wa kitaaluma watumishi hao.

Alieleza kufuatia Mkutano wa Chama cha Menejimenti ya Makatibu Mahsusi (TAPSEA) na Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka (TRAMPA) uliofanyika Mei 27 mwaka huu maeneo ya Fumba, Zanzibar kuna baadhi ya wakuu wa taasisi za Umma walishindwa kuwapa ruhusa watumishi wao ya kushiriki kwenye mkutano huo jambo aliloliomba kwa Serikali kutoendelea tena ili kuwapa uwezo watumishi wao kushiriki kwenye mikutano mkubwa kama hiyo kwani inawainua kifikra, weledi na kuwajengea ufanisi kwenye taaluma zao.

Mrope alieleza tukio la mkutano mkubwa wa Mei 27, limeandika historia mpya kwenye kumbukumba ya kada yao pia wameuita ni ushindi kwao kwa kufanikiwa kukutana pamoja wana taaluma wa kada ya watunza kumbukumbu zaidi ya 500.Mwenyekiti huyo wa TRAMPA alimueleza Dk. Mwinyi Chama chao hakisindikizi kwa Serikali wala kujihusisha na shughuli zozote nje ya chama chao.

Aidha, wanachama hao wa TRAMPA walitumia fursa hiyo kumkaribisha Rais Dk. Mwinyi kuwa Mwanachama wa chama hicho kwani mlezi wa chama hicho ni Mzee Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, awamu ya pili.Chama cha TRAMPA kilipata usajili wake namba SA 19596, tokea 29 Agosti mwaka 2014 kutoka kwa msajili wa vyama vya kijamii, Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi, kilianzishwa kwa lengo la kuwaunganisha wataalamu wa kumbukumbu na nyaraka Tanzania.