RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali inakusudia kuangalia maeneo ya kuingiza vipato ambapo wafanyabiashara wa India watashirikiana na Zanzibar kuendeleza sekta hiyo kwa maslahi ya wananchi wa nchi mbili hizo.Dk. Mwinyi amesema hayo Ikulu Zanzibar alipozungumza na ujumbe wa ngazi za juu kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya India, ulioongozwa na Katibu Mkuu wa Idara ya Ushirikiano kati ya India na Bara la Afrika Dammu Ravi.
Amesema Serikali itaangalia kwa kina maeneo yanayoweza kuingiza vipato ambapo wafanyabiashara wa India watashirkiana na kufanya kazi pamoja na wenzao wa Zanzibar ili kuendeleza sekta hiyo na kuleta maslahi kwa wananchi wa nchi mbili hizo.Dk. Mwinyi alieleza kuwa Serikali imekuwa ikifanya kila juhudi kutekeleza dhana ya Uchumi wa Buluu, hivyo akaiomba nchi hiyo kuanzisha kituo cha IT kwa kuzingatia uwepo wa soko kubwa hapa nchini kwa vile Zanzibar ni nchi ya kutoa huduma, hatua aliyosema itazalisha ajira.
Alisema pia kuna umuhimu wa kufungua hospitali maalum hapa nchini kwa ajili ya watalii ambao wamekuwa wakizuru kila mwaka kwa kiwango kikubwa.Aidha, alipongeza azma ya India ya kufungua Tawi la Hospitali ya Apollo hapa nchini katika eneo la Masaki Jijini Dar es Salaam, hatua itakayosaidia kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma bora za matibabu.
Dk. Mwinyi alitumia fuyrsa hiyo kupongeza uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya India na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, pamoja na misaada mbali mbali ya kiuchumi na kijamii ambapo nchi hiyo imekuwa ikiisadia Zanzibar, ikiwemo miradi ya huduma za maji safi na Salama ambapo kwa kiasi kikubwa itapunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo.
Nae, Katibu Mkuu wa Idara ya ushirikiano kati ya India na Bara la Afrika Dammu Ravi, amesema Serikali ya India inalenga kuimarisha ushirikiano wa muda uliopo kati yake na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kupitia nyanja mbali mbali, ikiwemo za biashara.Alisema India ina wataalamu wa kutosha katika sekta ya Uchumi wa Buluu, hivyo akaiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kubainisha maeneo ambapo Taifa hilo litaweza kuisaidia.
Aidha, Katibu huyo alisema nchi hiyo inalenga kupanua wigo wa mashirkiano kwa kuongeza fursa za masomo kupitia nyanja mbali mbali.Alisema wakati akiwa nchini alipata fursa ya kutembelea miradi mitatu ya maji inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbali kupitia ufadhili wa nchi hiyo na hivyo akaharakisha utekelezaji wake ili awamu nyingine ya miradi ya maji iweze kufanyika.
Katibu huyo alibainisha hatua zinazochukuliwa na India ili kufanikisha ujenzi wa Hospitali kubwa katika eneo la Masaki Jijini Dar es Salaam, ikiwa ni Tawi la Hospitali kubwa nchini humo ya Apollo