RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi   Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuongeza Bajeti ya Wizara ya Afya kadri hali ya Uchumi itakavyoimarika, ili kuhakikisha inatoa huduma bora za Afya nchini kote.Dk. Mwinyi amesema hayo katika uzinduzi wa ripoti ya ufuatiliaji wa mkataba wa Nairobi , kuhusu mkutano wa kimataifa wa idadi ya watu na maendeleo,  wenye lengo la kusimamia utekelezaji wa makubaliano kuhusu utoaji huduma bora kwa akinamama na watoto, hususuan katika masuala ya uzazi, uliofanyika Hoteli ya Melia Kiwengwa Mkoa Kaskazini Unguja.

Amesema katika mwaka huu wa Fedha wa 2022 Serikali imeongeza bajeti ya Wizara ya Afya kwa asilimia 8.3% kutoka asiliamia 7.7% iliotengwa katika mwaka wa fedha wa 2019/2020,  ikiwa ni juhudi za Serikali kufikia Azimio la Abuja la asilimia 15%.Alisema ongezeko hilo la bajeti limeweza kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za Afya katika nyanja tofauti, ikiwemo huduma za mama na mtoto, huduma za watoto na vijana pamoja na uzazi wa mpango kwa jamii ya Wazanzibari kote nchini bila malipo.

Alisema hivi sasa wananchi wote wanaweza kupata huduma bora za Afya katika eneo lisilozidi kilomita tano kutoka maakazi ya kudumu ya mwananchi, huku Serikali ikiwa njiani kukamilisha mpango wa Bima ya Afya.Dk. Mwinyi alisema kwa msaada wa washirika wa maendeleo Serikali inaendelea kuandaa mfumo wa afya ,  kujenga miundo mbinu ya Afya , kuajiri rasilimali watu , sambamba na kupata bidhaa zaidi za afya ili kuweza kutoa huduma bora za afya mijini na vijijini.

Aidha, alisema juhudi zinafanyika kuongeza upatikanaji wa elimu ya kina ya umri wa kujamiiana na uzazi kwa vijana wanaosoma na wasiosoma, ili kuzuia pamoja na kukabiliana na viwango vya juu vya vifo vya uzazi, magonjwa na mimba za utotoni ambazo zimekuwa zikiendeleea kujiri licha ya juhudi mbali mbali za Serikali.

Alisema pia serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa inafanyakazi kwa bidii kukomesha ukatili wa kijinsia wa aina zote , zikiwemo mimba za utotoni.Alieleza kuwa sheria, sera na mikakati iliopo imeimarishwa ili kuakisi malengo yaliowekwa katika ngazi za Kimataifa, kikanda na kitaifa.