RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itafanya kila juhudi kuhakikisha inasaidia upatikanaji wa usafiri pamoja na vifaa vya mawasiliano kwa ajili ya Jeshi la Polisi Zanzibar ili kuliwezesha kufanya kazi kwa ufanisi.

Dk. Mwinyi amesema hayo Ikulu Zanzibar, alipozungumza na Kamishna mpya wa Polisi Zanzibar CP Hamad Khamis Hamad, aliefika kujitambulisha.

Amesema pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa na dhima ya moja kwa moja kushughulikia masuala ya Usafiri na mawasiliano kwa Jeshi la Polisi Zanzibar, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaifanyia kazi changamoto ya upungufu wa magari pamoja na vifaa vya Mawasiliano   inayolikabili Jeshi hilo ili liweze kufanya kazi zake kwa ufanisi.

Alisema Serikali itaendelea kushirikiana kikamilifu na uongozi wa Jeshi hilo, huku akimpongeza Kamishna huyo kwa uteuzi huo.

Aidha, alimpongeza Kamishna Hamad kwa kukabidhiwa jukumu hilo, ikizingatiwa uzoefu wa kutosha alionao pamoja na na kuifahamu vyema Zanzibar katika masuala mbali mbali, yakiwemo ya kiuhalifu.

Nae, Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Hamad Khamis Hamad alimuomba Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Mwinyi kuangalia uwezekano wa kusaidia upatikanaji wa Usafiri pamoja na vifaa vya mawasiliano pale hali itakaporuhusu, ili kuliwezesha Jeshi hilo kutekeleza vyema majukumu yake ya kukabiliana na uhalifu.

Alisema Jeshi la Polisi Zanzibar, kama ilivyo kwa Jeshi la Polisi Tanzania, linakabiliwa na changamoto mbali mbali, ikiwemo ya usafiri na upungufu wa vifaa, hususan vya mawasiliano.

Alisema upatikianaji wa vifaa hivyo ni muhimu katika kukabiliana na makosa mbali mbali, akibainisha huwazesha askari kufika maeneo ya matukio wa wakati muafaka.

Alisema katika kipindi hiki Uongozi wa Jeshi la Polisi Zanzibar unaendelea kushughulikia mradi wa Ujenzi wa majengo mbali mbali, ikiwemo nyumba za Makamanda wa Polisi wa Mikoa ya Kusini na Kaskazini Unguja, kituo cha Polisi Mkokotoni pamoja na ukarabati wa majengo ya Polisi Ziwani Unguja.

Aidha, CP Hamad alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri hya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi kwa uteuzi wake na kubainisha faraja kubwa aliyonayo kutokana uteuzi huo, huku akisiistiza azma yake ya kushirikiana kikamilifu na taasisi na Vikosi vya SMZ katika kukabiliana na uhalifu nchini.

Wakati huo huo;  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi alizungumza na Balozi na Naibu Mwakilishi wa Kudumu Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Dkt. Suleiman Haji aliefika Ikulu kumuaga.

Alimtaka Balozi huyo kuangalia fursa zitakazopatikana katika kituo chake cha kazi na kusaidia kuinua uchumi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kupitia nyanja mbali mbali, ikiwemo ya Uwekezaji pamoja na ile ya kujenga uwezo.

Alisema Kituo hicho kina fursa pana kutokana na kutembelewa na watu kutoka Mataifa mbali mbali Duniani, hivyo akamtaka kuikumbuka Zanzibar kwa jicho la pekee.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imefarijika sana na Uwakilishi wa Balozi huyo katika kituo hicho.

Mapema, Balozi na Naibu Mwakilishi wa Kudumu Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Dkt. Suleiman Haji aliahidi kutumia nguvu, maarifa na juhudi zake zote ili kutekeleza vyema majukumu yake na kuiletea Maendeleo Tanzania.

Alitoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi kwa uteuzi wake wa kushika wadhifa huo. 

Katika hatua nyengine akizungumza na waandishi wa habari, Mwakilishi huyo ambae muda mfupi ujao anatarajiwa kuripoti katika Kituo chake cha kazi Jijiji New York Marekani, alisema kituo hicho kina fursa nyingi zinazoweza kuinufaisha Tanzania endapo zitatumika vizuri, ikiwemo suala la ufadhili katiika sekta ya Uchumi wa Buluu ambapo wavuvi, wafanya biashara na wakulima wa mwani wataweza kunufaika.

Alilitaja eneo jengine ambalo Zanzibar, ikiwa nchi ya Kisiwa itaweza kunufaika ni upatikanaji wa fedha katika kukabiliana na athari za kimazingira, akibainisha maeneo mbali mbali ya Visiiwa vya Unguja na Pemba kukabiliwa na hali mbaya ya kimazingira kutoka na uvamizi wa maji chumvi.

Aidha, alisema anakusudia kufanya juhudi ili kuhakikisha Watalii wa madaraja ya juu kutoka Marekani wanakuja nchini, na hivyo akatumia fursa hiyo kuitaka Serikali kujipanga kwa kuwa na miundo mbinu bora ili kuvutia watalii hao.

Balozi Suleiman alisema Wa-Tanzania wana fursa pana ya kufundisha Lugha ya Kiswahili nchini Marekani kwa kuzingatia uwepo wa Vyuo vikuu kadhaa vinavyohitaji huduma hizo, hivyo akaiomba Serikali kupitia Baraza la kiswahili (BAKIZA) kujidhatiti katika suala la kuzalisha walimu wengi wenye uwezo wa kufundisha lugha hiyo.