RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema, Zanzibar bado inahitaji wawekezaji zaidi kwani yapo maeneo mengi yenye fursa za uwekezaji ambayo hayajafikiwa na kutangazwa kimataifa.Rais Dk. Mwinyi ameeleza hayo Ikulu, Zanzibar alipokutana na timu ya wawekezaji kutoka bara Asia waliofika kueleza lengo la ujio wao kwa Zanzibar.

Amewahakikisha wawekezaji hao kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itawapa ushirikiano wa kutosha na kufungua milango mipya ya uwekezaji na kudumisha ushirikiano.Rais Dk. Mwinyi ameyataja maeneo yanayohitaji uwekezaji zaidi ni pamoja na utalii wa mikutano, michezo, utalii wa afya na utalii wa matamasha na kuwahimiza wawekezaji hao wajikite kwa utekelezaji wa haraka wa dhamira yao kwani Serikali ipo tayari kufanikisha azma zao.

Akizungumzia kilimo cha viungo vya asili vya Zanzibar (Spices) alisema, ni eneo muhimu ambalo Serikali inalipa kipaumbele na kuwashauri wawekezaji hao kuliangalia kwa karibu kutokana na Zanzibar kuwa na utajiri wa bidhaa hizo ambazo bado hazijaingia kwenye soko la Asia.

Eneo jengine ambalo Rais Dk. Mwinyi aliloligusia ni la uandaaji wa Filamu ambalo India imefanikiwa kwa kiasi kikubwa na kuwasisitiza kuangalia uwezekano wa kutoa mafunzo kwa waandaji wa filamu wazalendo na pia kuwaleta wasanii mashuhuri wa India kuja kuandaa filamu zao hapa nchini.

Alisema, Zanzibar inahitaji kuwa na hoteli za Daraja la juu zaidi akitolea mfano wa hoteli ya “Taj” iliopo India kujengwa Zanzibar huku akuwahakikishia Serikali imejipanga vizuri dhidi ya urasimu ili kufanikisha jambo hilo.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrik Ramadhan Soraga amesema tayari Wizara imezungumza na timu ya wawekezaji hao kuhusu kuitangaza Zanzibar kwenye ukanda wa bara Asia na kutafuta soko la uhakika la bidhaa zinazozalishwa nchini.

Naye, Mratibu wa ugeni huo, Rajiv Desai ambae pia ni Meneja Mkuu wa Kampuni ya Utalii ya ‘Swahili Safari’ amesema kampuni yake imeandaa mkakati maalum wa kuwaunganisha wawekezaji kutoka Dubai na India kuja kuwekeza Zanzibar kutokana na kuvutiwa kwa maumbile ya kijiografia yenye ushawishi wa utaalii na ukarimu wa Wazanzibari.

Katika hafla hiyo kulizinduliwa Jarida la “BlitzIndia” lenye nia ya kuitangaza Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kimataifa kwenye nyanja za uchumi, maendeleo, utalii, sana na utamaduni, ambapo Rais Dk. Mwinyi alikabidhiwa nakala ya Jarida hilo lilizozinduliwa rasmi hapo Ikulu.