RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar ina wagonjwa wengi wenye matatizo mbali mbali ya macho, hivyo misaada kutoka taasisi za ndani na nje ya nchi ni muhimu.
Dk. Mwinyi amesema hayo wakati alipozungumza na kikundi cha madaktari kutoka taasisi ya ‘Association Vission-for-Puma (Germany) kilichoongozwa na Dk. Frank Klemm, kilichofika Ikulu Zanzibar baada ya kumaliza zoezi la utoaji wa huduma na tiba ya macho katika Hospitali ya KMKM Kibweni, Mkoa Mjini Magharibi Unguja.
Dk. Mwinyi alisema pamoja na Zanzibar kuwa na Hospitali ya macho katika Hospitali kuu ya Mnazi mmoja, bado inakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa vifaa muhimu pamoja na wataalamu , mambo yatakayofanikisha utoaji bora wa huduma za macho nchini.
Alitumia fursa hiyo kuipongeza timu ya madaktari hao kwa ujio wao pamoja na kazi kubwa waliyofanya ya kuwapatia huduma mbali mbali wagonjwa.
Alisema serikali itaangalia namna ya kuendeleza ushirikiano ulioanza na taasisi hiyo katika siku zijazo.
Nae, Kiongozi wa timu hiyo ya madaktari kutoka Taasisi ya ‘Association Vission –for-Puma (Germany) Dk. Fank Klemm alipongeza mashirikiano makubwa waliyopata kutoka Uongozi wa Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM) pamoja na madaktari wa Hospitali ya KMKM Kibweni katika kipindi chote walipokuwa nchini.
Alisema wagonjwa 100 walipatiwa huduma mbali mbali za macho katika Kliniki hiyo iliodumu kwa siku 12, huku wengine wakipatiwa miwani ya macho.