RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikano uliopo kati yake na Australia kwa maslahi ya nchi mbili hizo.Dk.Mwinyi amesema hayo Ikulu Zanzibar, alipozungumza na Balozi wa Australia nchini Tanzania Luke Williams, ambae pia anaziwakilisha nchi za Kenya, Rwanda, Somalia na Burundi, ambapo amefika kwa ajili ya kujitambulisha.

Alisema kuna umuhimu kwa nchi mbili hizo kuendeleza ushirikiano uliopo wakati huu Zanzibar ikiweka kipaumbele katika kuimarisha uchumi wake kupitia Sekta za Uchumi wa Buluu, unaohusisha sekta za Utalii, kilimo cha mwani na Uvuvi.Dk. Mwinyi alitumia fursa kuiomba Autralia kusaidia uimarishaji wa sekta hizo na kumpongeza Balozi huyo kwa dhamira yake ya kusaidia Zanzibar katika sekta ya kilimo.

Nae, Balozi wa Australia nchini Tanzania, Luke Williams aliahidi kuendeleza ushirikano uliopo kati ya Australia na Tanzania pamoja na kuunga mkono azma ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya Uchumi wa Buluu kwa kuzingatia uwepo wa fursa mbali mbali.Alisema Zanzibar ni kituo muhimu cha utalii kutokana na historia yake, kuwa na mandhari ya kuvutia pamoja na Utamaduni wa watu wake.

Alimhakikisha Rais Dk. Mwinyi kuwa atafanya juhudi kusaidia uendelezaji wa kilimo kwa kuzingatia Zanzibar ina utajiri katika uzalishaji wa viungo.