Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza umuhimu wa kufanya siasa za kistaarabu nchini kwa kuweka mbele maslahi ya Taifa sambamba na kudumisha amani Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Kikosi Kazi cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan cha kuratibu Maoni ya Wadau wa Demokrasia ya Vyama vingi vya Siasa kikiongozwa na Mwenyekiti wake Professa Rwekaza Mukandala.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba hakuna jambo kubwa katika Taifa lolote duniani isipokuwa amani ambayo inakuja kwa kufanya siasa za kistaarabu.Alitoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuunda kikosi kazi hicho ili kikusanye maoni na baadae kitoe mapendekezo kwa Serikali zote mbili ambapo Serikali nazo ziweze kuyafanyia kazi ili kuweza kuhakikisha nchi inadumu katika amani na siasa zinafanywa kistaaru kwa maslahi ya nchi.
Hivyo. alisisiatiza haja kwa Watanzania wote kuunga mkono juhudi hizo hususan vyama vya siasa hatua ambayo itaondokana na changamoto zilizopo.Rais Dk. Mwinyi alitoa shukurani kwa Kikosi Kazi hicho na kueleza haja ya kukamilisha kazi waliyoianza huku akikiahidi Kikosi kazi hicho, umma wa Watanzania na Wazanzibari wote kwamba mapendekezo yatakayoletwa na Kikosi Kazi hicho yatafanyiwa kazi ili kuweza kuondoakana na changamoto za utendaji wa siasa nchini.
Aidha, alieleza haja kwa Kikosi Kazi hicho kuendelea kukaribisha maoni na kuyakusanya kwa lengo la kuyafanyia kazi ambapo kati ya maeneo tisa yaliyoelezwa na Kikosi Kazi hicho matatu kati yake bado yana changamoto zaidi ikiwemo Katiba Mpya, Utaratibu wa Uchaguzi kwa ujumla wake na mikutano ya hadhara na ujumla wake.
Rais Dk. Mwinyi alichukua fursa hiyo kuviomba vyama vyengine vya siasa ambavyo havijaamua kuwa sehemu ya jambo hilo basi viamue kuingia kwa sababu lazima Watanzania wote wawe sehemu ya jambo hilo muhimu.Alisema kwamba njia nzuri za kutatua changamoto ni kupitia katika mijadala kama hiyo badala ya kuyatumia majukwa ya kisiasa na kuanza kutoa kushutuma kwa mwengine jambo ambalo halileti amani katika nchi na kuvitaka vyama vyote vya siasa kuingia kwenye jambo hilo kwani hiyo ndio njia bora ya kutatua changamoto zilizopo.
Alikipongeza Kikosi Kazi hicho kwa kufanya kazi kwa uzalendo na kusisitiza kwamba maslahi ya nchi ni vyema yakawekwa juu kuliko vyama vya siasa kwani nchi ni muhimu zaidi kwa lengo la kupata amani na maendeleo.Alieleza matumaini yake juu ya Kikosi hicho kutokana na mchanganyiko wa Wajumbe wake huku akieleza kwamba kutokana na migogoro inayojitokeza kila ikifika wakati wa uchaguzi hapa Zanzibar basi ni vyema wadadu wakubwa wa Kikosi Kazi hicho wakawa Wazanzibari pamoja na vyama vyote vya siasa hapa Zanzibar ambavyo vitakuwa sehemu ya maoni hasa katika kuelekea uchaguzi wa mwaka 2025.
Alieleza kwamba si vyema kuona yale yaliyojitokeaza siku za nyuma yanajirejea kwani wakati huu ndio muwafaka wa kueleza changamoto zilizopo na kuzifanyia kazi ili ifikapo mwaka 2025 mambo yote yawe yamewekwa vizuri ili kuweza kuingia katika uchaguzi kwa amani na usalma.Alisema kwamba amani iliyiopo hivi sasa haiwezi kudumu kama bado kuna baadhi ya maneno ya huku na kule ambayo hayatowekwa sawa na kueleza haja ya kuwepo ushiriki kwa vyama vyote ili mambo yakae sawa kwani kazi hio ikikamilika itasaidia siasa nchini.
Akitoa taarifa ya Kikosi Kazi hicho, Mwenyekiti wake Professa Rwekaza Mukandala alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa juhudi zake kubwa anazozifanya katika kuleta maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa hapa Zanzibar.alitoa shukurani kwa hotuba ya Rais Dk. Mwinyi ya ufunguzi ambayo ilitoa mwongozo wa kufanya siasa za kistaarbu hapa nchini huku ikizingatiwa maslahi ya Taifa ikiwemo kudumisha amani,utulivu na umoja wa kitaifa.
“Kwetu sisi Kikosi Kazi hotuba ya uzinduzi pamoja na ile uliyoitoa wakati wa kufunga mkotano wa wadadu tarehe 17 Disemba 2022 huko Dodoma, tunazitumia kuwa ni dira ya kazi zetu”,alisema Professa Mukandala.Katika taarifa hiyo alieleza kazi walizokwisha kuzifanya ikiwemo kupitia hadidu za rejea ili kupata uelewa wa pamoja, kuchambua maoni na mapendekezo yalitotolewa katika mkutano wa wadau na kuainisha masuala muhimu ya kazi.
Kazi nyengine ni kuandaa Mpango Kazi wa Kikosi Kazi wa kufanyia kazi masuala yaliyoanishwa, kuchambua suala la mikutano ya hadhara na mikutano ya ndani ya vyama vya siasa na kuwasilisha mapendekezo ya awali kwa Rais wa Jamhuri ya Muunganow a Tanzania.Jengine alieleza ni kukaribisha wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa kuwasilisha maoni yao kwa Kikosi Kazi ili kupata maoni na mapendekezo zaidi na ufafanuzi wa maoni na mapendekezo yaliyokwisha tolewa.
Alieleza masuala makuu tisa ya kufanyiwa kazi kutokana na mapendekezo ya washiriki wa mkutano wa wadau wa tarehe 15-17 Disemba 2022 yakiwemo mikutano ya hadhara na ndani ya vyama vya siasa, masuala yanayohusu uchaguzi, mfumo wa maridhiano ili kudumisha haki, amani, utulivu na umoja wa kitaifa, ushiriki wa wanawake na makundi maalum katika siasa na demokrasia ya vyama vingi vya siasa, elimu ya uraia, rushwa na maadili katika siasa na uchaguzi, ruzuku ya Serikali kwa vyama vya siasa, uhusiano wa siasa na Mawasiliano kwa umma pamoja na Katiba mpya.
Nao baadhi ya Wajumbe wa Kikosi kazi hicho walipata fursa ya kutoa maelezo yao ambapo walimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kupata fursa hiyo na kueleza kwamba hadidu rejea alizowapa wanaizifanyia kazi.Walieleza kwamba wanafanya kazi hizo wakiwa wameuvaa uzalendo kwa azma ya kuliletea maslahi Taifa kwa kizazi cha leo na kijacho.Walieleza kwamba Kikosi Kazi hicho kimewashirikisha watu wa aina zote na kumpongeza Rais Dk. Mwinyi na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuunda Kikosi kazi hicho ambacho kimeweza kuifanya Tanzania kuweza kushughulikia mambo yake ya kisiasa wenyewe.
Mapema akitoa utambulisho wa Kikosi Kazi hichoNaibu Msajili wa Vyama vya Siasa Mohamed Ali Ahmed alipongeza mashirikiano mazuri waliyoyapata kutoka Ofisi ya Rais Ikulu Zanzibar huku akieleza muendelezo wa kazi za Kikosi hicho tokea pale alipokizindua Rais Dk. Mwinyi mnamo Januari 10.2022