RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa wito kwa Watendaji wa Serikali kuhakikisha wanashughulikia ipasavyo malalamiko yanayowasilishwa na wananchi kupitia Mfumo wa Sema na Rais Mwinyi (SNR) ili mfumo huo uweze kuleta tija na kuwa endelevu.Dk. Mwinyi ametoa wito huo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipozungumza na watendaji wa Kitengo cha SNR Ofisi ya Rais Ikulu, ambapo pamoja na mambo mengine alipokea taarifa za kiutendaji kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu mfumo huo uzinduliwe February 27, 2021.

Alisema wasimamizi wa mfumo huo katika taasisi na Wizara za Serikali wanapaswa kuhakikisha Maofisa wanaoshughulikia mfumo huo wanatimiza wajibu wao ipasavyo na kusema Serrikali inakusudia kuimarisha mfumo huo pamoja na kuwa na utaratibu wa kutoa taarifa kwa umma siku zijazo.Alisema lengo la Serikali la kuanzisha mfumo huo ni kuwawezesha wananchi kuwasilisha malalamiko yao Serikalini ili yaweze kutafutiwa njia nzuri ya kuyashughulikia na kuyapatia ufumbuzi.

Rais Dk. Mwinyi aliwahakikishia wananchi kuwa mfumo wa SNR umepata mafanikio mazuri na kusema Serikali itaendelea na juhudi za kuzitafutia ufumbuzi changamooto mbali mbali zinazowasilishwa ambazo hadi sasa bado hazijapatiwa ufumbuzi.“Katika kipindi cha mwaka mmoja kumekuwepo mafanikio makubwa ya kuzipatia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazowasilishwa, mbali na kuwepo kwa changamoto za mfumo pamoja na utendaji katika taasisi na Wizara za Serikali”, alisema.


Alisema dhamira ya serikali ni kuyapatia ufumbuzi malalamiko yote yanayowasilishwa , hivyo akataka kuwepo mashirikiano kutoka kwa kila mtu.

Dk. Mwinyi ametumia fursa hiyo kuwapongeza Watendaji wa kitengo cha SNR Ofisi ya Rais Ikulu, pamoja na watendaji wa SNR walioko katika Taasisi na Wizara mbali mbali za Serikali kwa kazi nzuri wanayofanya, huku akibainisha malalamiko mengi yakiwa yamefanyiwa kazi.Alisema katika kipindi hicho asilimia 73 ya malalamiko yaliowasilishwa yamewweza kupatiwa ufumbuzi.

Nae, Mkuu wa kitengo cha SNR Ofisi ya Rais Ikulu, Haji Makame alisema katika kipindi hicho cha mwaka mmoja, Ofisi hiyo iliweza kupokea jumla ya malalamiko 6,675 kutoka kwa wananchi mbali mbali Unguja na Pemba na kuyafanyia kazi.Alisema hadi kufikia sasa jumla ya malalamiko 4,856 ikiwa sawa na asilimia 73% yaliweza kupatiwa ufumbuzi, huku malalamiko 1,819 sawa na asilimia 27 yakiwa yanaendelea kufuatiliwa.

Aidha alizitaja Wizara za TAMISEMI, Elimu na Mafunzo ya Amali pamoja na Wizara za Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na watoto kuwa zinaongoza miongozi mwa Wizara na Taasisi za Serikali zilizolalamikiwa.Alieleza kuwa sekta za Umeme, Maji , Ardhi pamoja na Udhalilishaji kushika hatamu miongoni mwa kadhia ziliozibuwa migogoro. sintofahamu au makosa katika jamii. 

Makame alisema katika malalamiko hayo yaliowasilishwa kulikuwa na Viongozi na watendaji wakuu mbali mbali wa Seriklai waliolalamikiwa kuhusika katika matukio tofauti , ikiwemo ubadhirifu wa mali za Serikali.