RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameupongeza Mfuko wa Mawasiliano kwa wote kwa kuwekeza zaidi ya Shilingi Bilioni 6.9 kwa ajili ya ujenzi wa Minara ya Mawasiliano ili kuwawezesha wananchi wa maeneo mbali mbali hapa nchini kupata mawasiliano ya uhakika.

Dk, Mwinyi ametoa pongezi hizo katika hafla ya uznduzi wa mradi wa Mnara wa Mawasiliano uliopo Donge Mtambile, Mkoa wa Kaskazini Unguja, akiwa katika muendelezo wa ziara yake ya kuitembelea miradi mbalimbali ya Maendeleo inayotekelezwa kupitia Fedha za ahueni ya Uviko -19, pamoja na miradi mingineyo.

Mnara huo ni mmoja miongoni mwa Minara 43 iliojengwa katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar, na 13 katika Mkoa wa Kaskazini Unguja chini ya Kampuni ya ZANTEL-TIGO.

Alisema uzinduzi wa mnara huo unaaakisi dhamira ya Serikali ya kuwaondolea changamoto wananchi wa maeneo mbali mbali ambao wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la kupata mawasiliano duni.

Alieleza kuwa Serikali imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta mbali mbali, ikiwemo Afya, Elimu, Umeme, Ujasiriamali pamoja na Uwezeshaji wananchi kiuchumi na akabainisha matarajio yake ya miradi hiyo kufunguliwa kabla ya sherehe za Mapinduzi.

Aidha, aliwataka wananchi wa Jimbo la Donge kujipanga na kutumia vyema fursa za kupata mikopo ili kuweza kuimarisha biashara zao, huku akibainisha kuwa eneo la Pangatupu limetengwa kwa ajili ya Viwanda, ikiwa ni hatua ya wananchi kupata ajira.

Katika hatua nyengine, Rais Dk. Mwinyi alifika eneo la Pangatupu na kuzindua mradi wa Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Kaskazini ‘B’ na akatumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa Wizara ya Afya na watendaji wake, Wakandarasi pamoja na washauri Elekezi kwa kazi nzuri ya kusimamia Hospitali za Wilaya hadi hivi sasa.

Alisema Serikali imepanga kufanya Mapinduzi makubwa ya utoaji wa huduma katika sekta ya Afya, ambapo kwa kuanzia inajenga Hospitali kubwa katika Wilaya zote za Unguja na Pemba pamoja na Hospitali ay mkoa iliopo Lumumba.

Alisema Serikali ina azma ya kujenga Hospitali ya kubwa ya Mkoa ndani ya Mkoa Kaskazini Unguja ambayo pamoja na mambo mengine itaendesha huduma za upasuaji.

Sambamba na hilo Dk. Mwinyi aliutaka uongozi wa Mkoa kufanya juhudi z akupata eneo kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Amali ndnai ya Mkoa.

Mapema Waziri wa Afya Ahmeid Nassor Mazrui alisema ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Kaskazini ‘B’ ni hatua muhimu katika kuimarisha huduma za Afya nchini.

Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Husssein Ali Mwinyi alifika nyumbani kwa Marehemu Mwalimu Fatuma Juma Khamis kwa ajili ya kutoa mkono wa pole.

Marehemu Fatuma Juma aliekuwa Mwalimu katika Skuli ya Mahonda, alifariki dunia leo baada ya kupata ajali ya kugongwa na gari katika eneo hilo la Mahonda. Mwenyezi Mungu aiweke roho ya Marehemu peponi – Amin