RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameutaka Uongozi wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Taasisi ya Sayansi za Bahari (IMS), kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kufanya kazi ya kuielimisha jamii dhana na dhamira ya Uchumi wa Buluu kwa ajili ya maendeleo ya nchi.Dk. Mwinyi ametoa wito huko Buyu Mkoa Mjini Magharibi alipozungumza katika Mahafali ya 52 Duru ya nne, ya Taasisi ya Sayansi za Bahari (IMS), Kampasi ya Buyu.
Akizungumza na Wahitimu, Viongozi wa Chuo pamoja na wnanchi Dk. Mwinyi alisema kuna umuhimu wa Uongozi wa Chuo hicho kushirkiana na Serikali na kufanya kazi ya ziada ya kuielimisha jamii juu ya dhana ya Uchumi wa Buluu na dhamira ya Serikali ya kuweka kipaumbele katika matumizi ya rasilimali za Bahari katika kuimarisha uchumi.
Alisema serikali itaendeleea kutoa ushirikiano na IMS katika kuimarisha sekta ya Uchumi wa Buluu unaozihusisha sekta za Uvuvi pamoja na Kilimo cha Mwani kwa kuamini kuwa Chuo hicho ni chanzo muhimu katika kuibuwa watalamu.
Aidha, Dk. Mwinyi alisema Serikali inatambua mchango mkubwa wa Taasisi za Elimu ya Juu nchini na kubainisha uwepo wa IMS kuwa ni fursa muhimu katika maendeleo ya sekta ya uchumi wa Buluu.
Alisema Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa IMS katika uimarishaji wa zao la Mwani, lenye kuzalisha ajira kwa kiwango kikubwa, hususan kwa akinamama.
Aliuahidi Uongozi wa Chuo hicho kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaifanyia matengenezo kwa kuiijumuisha barabara chakavu iendayo Chuoni huko kupitia mradi wa ujenzi wa barabara za Ndani unaotekelezwa na Serikali.
Aidha, alitoa maelekezo kwa Wizara ya Ardhi, makaazi na Maendeleo kushuhulikia upatikanaji wa Hatimiliki ya Chuo hicho.
Katika hatua nyengine, alitoa wito kwa wahitimu hao kutotosheka na kiwango cha elimu walichofikia na badala yake kutumia taaluma na maarifa waliyopata ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Nae, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete akiakhirisha Mahafali hayo alisema tangu mwaka 2019 Kampasi ya Buyu ilianza kuchukua wanafunzi wa shahada ya awali na hivyo kuingia katika utaratibu wa kufanya mahafali kuanzia mwaka huu, lengo likiwa ni kutangaza shughuli za chuo hicho pamoja na kuwahamasisha vijana wanaomaliza masomo ya kidato cha sita (F.VI) kujiunga na chuo kwa masomo ya Chuo Kikuu.
Alimshukuru Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi kwa ahadi yakuzipatia ufumbui changamoto mbali mbali zinazokikabili chuo hicho, ikiwemo uchakavu wa barabara, hatua itakayorahisisha safari za wanafunzi wafanyakazi kutoka Hosteli hadi Chuoni.
Dk. Kikwete alisema chuo hicho kimepanga kushirikiana na Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA)kwa maslahi ya Taifa, na akabainisha azma ya Chuo hicho ya kuandaa Kongamano kubwa la Kimataifa litakalowashishirikishs wataalamu wabobezi kuhusu Uchumi wa Buluu, ili wananchi waweze kufahamu dhana nzima ya Uchumi wa Buluu.
Mapema, Makamu Mkuu wa Chuo Pro. William A.L. Anangisye alisema katika kuunga mkono juhudi na Dira ya Serikali zote mbili katika kuendeleza Uchumi wa Buluu kwa kutoa wataalamu wa kujenga uwezo wa kitaasisi, IMS imejizatiti katika utoaji wa mafyunzo ya utafiti ili kuchochea kasi ya matumizii endelevu ya bahari yatakayotoa mchango chanya katika uchumi wa nchi na maendeleeo ya kijamii.
Alisema taasisi ina mpango wa kulifanya jengo la Mizingani kuwa kituo Bobevu cha utafiti wa masuala ya Uvuvi, ikiwa mwendelezo wa juhudi zinazoendelea kwenye kituo cha utafiti kilichopo Pangani Tanga kinachojishughulisha na utafiti wa mbegu na chakula bora kwa ajili ya ufugaji wa samaki.
Alisem kwa muda wote huo Chuo kinajivunia mafanikio makubwa yaliopatikana, ikiwemo uanzishwaji na uendelezwaji waa kilimo cha mwani ambacho kimeenea kote nchini t na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya tatu Dunian kwa uzalishaji wa mwani.
Aidha, alisema IMS imefanikiwa kuanzisha utafiti mkubwa wa uzalishaji wa mbegu bora za samaki, ambapo kwa kuanzia kilianza na samaki aina ya Perege, Kolekole pamoja na Majongoo bahari.
Alieleza kuwa mafanikio ya wahitimu yametokana na michango iliyotolewa kwa nyakati tofauti na wadau , ikiwemo serikali zote mbili, mashirka kutoka nchi rafiki, asasi za kiraia, wafadhili pamoja na familia.
Hata hivyo alisema Chuo hicho kinakabilwia na changamoto mbali mbali, ikiwemo ile ya uchakavu wa barabara inayoelekea chuoni.
Pro. Anangisye aliwataka wahitimu hao kutumia elimu waliyoipata kama ushawishi kwa wadau wote wanaowazunguka na kuwa chachu ya mabadiliko katika jamii, kwa kufahamu kuwa elimu hiyo ni mali ya umma.
Aidha, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Balozi Mwanaidi Sanare Maajar alisema ni matarajio ya Baraza hilo kuwu wahitimu hao watakuwa chachu katika kuchochea ukuaji wa sekta mbali mbali za Uchumi wa Buluu, kwa kuongeza uwezo na Ufanisi wa kitaasisi, uwezo wa kujiajiri kupitia taaluma na maarifa waliyopata.
Alisema Baraza la Chuo linafarijika na hatua mbali mbali zinazochukuliwa na Uongozi wa Chuo pamoja na Serikali katika kuboresha miundombinu katika taasisi hiyo (IMS), ikiwemo Ujenzi wa majengo mbali mbali pamoja na Bweni la Wanafunzi kupitia mradi wa HEET, unaokwenda sambamba na ukarabati wa jengo la Mizingani lililoathiriwa kwa kwiango kikubwa na ajali ya moto.
Mahafali ya 52 Duru ya nne yamewahusisha wahitimu 38, kati yao wahitimu wanne wa Shahada ya Udaktari wa Falsafa katika Sayansi za Bahari, wahitimu saba wa Shahada ya Umahiri wa Sayansi katika Sayansi ya Bahari pamoja na wahitimu 27 wa Shahada ya Awali ya sayansi za Bahari.