RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameutaka Uongozi wa Wilaya na Mkoa Kaskazini Unguja kushirikiana na kiuhakikisha wananchi wa Mkoa huo wanasaidiwa kupatiwa zana, vifaa, elimu pamoja na mitaji ili kufanikisha dhana ya uchumi wa Buluu, hususan kupitia sekta ya uvuvi.Dk. Mwinyi amesema hayo Hoteli ya Melia ilioko Kiwengwa Mkoa Kaskazini Unguja katika hafla ya Majumuisho ya ziara yake ya kutembelea na kukagua miradi mbali mbali ya Maendeleo katika Mkoa huo, inayotekelezwa kupitia Fedha za Ahueni ya Uviko – 19, na miradi mingineyo.
Amesema kuna umuhimu kwa viongozi hao kushirikiana kwa kuwapatia mambo hayo ili waweze kufanikisha kikamilifu dhana ya uchumi wa Buluu, kupitia sekta za Utalii, uvuvi, kilimo cha mwani pamoja na fukwe na rasilimali nyingine za bahari.Alisema Uchumi wa Buluu ni eneo ambalo Serikali imelipa kipaumbele, huku akibainisha azma iliopo ya kujenga Bandari kubwa na Kisasa katika eneo la Mangapwani kuwa inalenga kuibua ajira na kuimarisha uchumi wa taifa.
“Muda sio mrefu nitatoa taarifa ya lini ujenzi wa Bandari utaanza”, alisema.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi aliyataka Mabaraza ya Miji kuhakikisha yanaleta maendeleo kwa wananchi kwa kutumia fedha wanazokusanya kwa ajili miradi ya mendeleo.
Alisema, amefurahishwa na hali ya ulinzi na usama wa Mkoa huo ilivyo na kubainisha kuwa amani ndio mtaji wa kwanza wa nchi, hivyo kuna haja ya kudhibiti vitendo vya uhalifu , hususan kwa watalii.
Kuhusiana na Kisiwa cha Tumbatu Dk. Mwinyi aliwataka Mawaziri wanaohusiana na sekta za Maji, Elimu, Afya, Ujasiariamali na Uwekezaji kushirikiana ili kutimiza ahadi mbali mbali alizoweka kwa wananchi.
Alisema kuna umuhimu wa kushirikiana ili kusaidia maendeleo ya kisiwa hicho, kutokana na mazingira ya kisiwa kilivyo, huku akibainisha baadhi ya ahadi hizo kuwa ni pamoja na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ndogo Tumbatu, ujenzi wa Gati, ujenzi wa Skuli ya Ghorofa , Kiwanja cha Mpira pamoja na kukamalisha ujenzi wa Tangi la Maji.
Katika hafla hiyo ya majumuisho, Dk. Mwinyi alipata fursa ya kuelezea utekelezaji wa miradi katika sekta mbali mbali, ikiwemo Afya, Elimu, Ujasiriamali pamoja na Uwezeshaji wananchi kiuchumi, ambazo zinatekelezwa kupitia fedha za Ahueni ya Covid – 19, na kusema ameridhishwa na utekelzaji wa miradi hiyo, sambamba na Kikipongeza kikosi cha Mafunzo kwa kazi nzuri na yenye kiwango.
Mapema, Rais Dk. Mwinyi alipata fursa ya kuzindua Madarasa manane katika Skuli ya Msingi Mahonda na kusema Wizara ya Elimu itatenga fedha maalum kwa ajili ya kuyafanyia ukarabati madarasa makongwe nchini kote.
Aidha, Dk. Mwinyi alifika katika Bonde la Mpunga Upenja na kupata taarifa ya maendeleo ya Mradi wa Miundombinu ya Umwagiliaji maji,na kumshukuru Mkandarasi wa Mradi huo kwa kuwa muungwana na kukubali kuzifanyia marekebisha kasoro zilizojitokeza katika utekelezaji wa mradi kwa kutumia fedha zake mwenyewe.
Aliitaka Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kusimamia vyema ugawaji wa vitalu katika Bonde hilo kwa kuwashirikisha wakulima, huku akiwahadharisha watendaji wa Serikali kutojihusisha na umiliki wa maeneo yanayogawiwa.
Nae, Mkuu wa Mkoa Kaskazini Unguja, Ayoub Mohamed Mahamoud alitoo shukurani kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kuwezesha mafanikio makubwa ya maendeleo mkoani humo kupitia miradi mbali mbali.
Alimshukuru Dk. Mwinyi kwa kuufungua Mkoa huo hususan katika Kisiwa cha Tumbatu, sambamba na kuunga mkono zma ya Serikali ya ujenzi wa Bandari ya Mangapwani, akibainisha hatua hiyo itawanufaisha kiuchumi wananachi wa maeneo yote.
Ziara hiyo ya Rais Dk.Mwinyi inaendelea tena kesho kwa kutembelea na kukaguwa miradi mbali mbali ya maendeleo katika Mkoa wa Kusini Unguja.