RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amewakaribisha Zanzibar wafanyabiashara wakubwa na wenye viwanda kutoka China.
Akizungumza na Makamo Mwenyekiti wa Shirikisho la wenye viwanda na wafanyabiashara wa China, Xu Lejiang na ujumbbe wa wafanyabiashara 15 Ikulu, Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi aliwaeleza wafanyabiashara hao, utalii ni fursa muhimu ya uwekezaji kwa Zanzibar.

Aliwaeleza utalii hasa wa hoteli na maeneo ya kupumzikia unafursa nyingi za uwekezaji, kwani Zanzibar ina maeneo mazuri ya fukwe nyeupe zinazowavutia wageni na watalii wengi.Kuhusu sekta ya Uchumi wa Buluu, Rais Dk. Mwinyi aliwakaribisha wafanyabiashara hao kuangalia fursa eneo hilo kwani Zanzibar mbali sekta ya Utalii inayoingiza asilimia 30 ya pato la taifa lakini uvuvi na ufugaji wa vifaranga vya samaki ni sekta muhimu pia kwa uchumi wa nchi, hivyo alilitaka Shirikisho la wenye viwanda na wafanyabiashara kutoka China kuangalia fursa za uwekezaji kwenye eneo hilo.

Pia, Rais Dk. Mwinyi aliwaeleza wageni hao maumbile ya visiwa vya Zanzibar vina fursa adhimu ya bandari, hivyo aliikaribisha China kuitumia fursa hiyo kwa uwekezaji pamoja na kutuma na kupokea mizigo kwa pande mbili hizo za ushirikiano.Akiizungumzia sekta ya Mafuta na Gesi, Rais Dk. Mwinyi pia alilitaka Shirikisho hilo la Wenyeviwana na wafanyabiashara la China kuangalia pia eneo hilo kwa uwekezaji.

Naye, bw. Xu Lejiang, alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba Shirikisho hilo la wenye viwanda na wafanyabiashara ni kubwa zaidi kwa China kwani limeyaweka pamoja zaidi ya makampuni makubwa na viwanda 700 wakiwemo wafanyabiashara wa madini, makampuni ya vifaa mbalimbali ikiwemo ujenzi na teknolojia, wafanyabiashara wakubwa na masuala ya kilimo kikubwa ambapo wengi wao wapo Zanzibar.

Kiongozi huyo alimuahidi Rais Dk. Mwinyi kuwashawishi wafanyabiashara wengi zaidi kuja kuwekeza Zanzibar huku ikiangaliwa Zanzibr na China inatimiza miaka 60 ya ushirikiano wao wa diplomasia pamoja na uhusiano wao wa kiuchumi, kisiasa na jamii.