Media » News and Events

Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka Mabalozi walioteuliwa hivi karibuni kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Zimbabwe, Zambia na Uholanzi; kufanya juhudi za kuitangaza Tanzania

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka Mabalozi walioteuliwa hivi karibuni kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Zimbabwe, Zambia na Uholanzi; kufanya juhudi za kuitangaza Tanzania pamoja na kuangalia fursa za kiuchumi.Dk. Mwinyi ametoa wito huo Ikulu Zanzibar, alipozungumza na ujumbe wa Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania, akiwemo Balozi Simon N. Siro (Zimbabwe), Let.Gen.Mathew E. Mkingule (Zambia) pamoja na Balozi Caroline Chipeta anaeiwakilisha Tanzania nchini Uholanzi,  waliofika Ikulu kwa ajili ya kuagana.

Amesema kuna umuhimu mkubwa kwa Mabalozi hao kuitangaza vyema Tanzania katika nchi hizo kwa kuendeleza ushirikiano mzuri uliopo pamoja na kuangalia fursa mbali mbali za kiuchumi zinazopatikana, ikiwemo za uuzaji bidhaa au utoaji wa huduma.

Alisema katika kutekeleza Diplomasia ya Uchumi, Serikali imeweka kipaumbele sekta za Uchumi wa Buluu kwa lengo la kukuza uchumi wake,  hivyo akasisitiza umuhimu wa kuzifanyia kazi fursa ziliomo katika sekta hizo; ikiwemo ya Uvuvi, mafuta na Gesi asilia na   nyenginezo.

Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumtaka Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi Caroline Chipeta kuweka nguvu ili kuongeza idadi ya Watalii wa nchi hiyo wanaozuru nchini.

Alisema kwa kipindi kirefu sasa, Zanzibar imekuwa ikipokea watalii wengi kutoka nchi za Ulaya, Ulaya Mashariki pamoja na Marekani, hivyo akabainisha umuhimu wa kuelekeza nguvu zaidi katika soko la watalii kutoka nchi za Scandanavia.

Aidha, Dk. Mwinyi alimtaka mabalozi hao kuchangamikia fursa za masoko ya mazao ya Karafuu na Viungo kwa kuwaunganisha wafanyabiashara wa nchi hiyo pamoja na wale wa Zanzibar.

Katika hatua nyengine, Dk. Mwinyi aliwataka Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi za Zimbabwe na Zambia kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa Kihistoria uliopo kwa kuangalia fursa za kibiashara zilizopo katika nchi hioz pamoja na kuzingatia suala la ulinzi na Usalama.

Nao,  Mabalozi hao kwa nyakati tofauti walimshukuru Rais Dk. Mwinyi kwa maelekezo aliyowapa na wakaahidi kuyafanyia kazi ili kuleta ustawi wa Tanzania na watu wake.

Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe Simon N. Siro alisema ataangalia kwa kina fursa za kiuchumi ziliopo nchini humo, hususan katika kilimo cha zao la Mahindi ili kubaini sababu za nchi hiyo kuzalisha bidhaa hiyo kwa kiwango kikubwa, sambamba na kuahidi kuangalia namna ya kuwaunganisha watalii wanaozuru nchi hiyo ili waweze kufika hadi Tanzania.

Nae, Balozi wa Tanzania nchini Zambia Let. Gen. Mathew E. Mkingule, alisema ataendeleza ushirkiano wa kihistoria uliopo kati ya Taifa hilo na Tanzania pamoja na kuangalia namna ya kuchakata mafuta yanayosafirishwa kupitia Bomba la Mafuta kutoka Dar es Salaam hadi Zambia pamoja na kuangalia fursa nyengine za kibiashara kupitia Reli ya Tazara.

Aidha, Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi Caroline Chipeta, alisema atafanya juhudi ili kuhakikisha idadi ya watalii wanaotoka Uhalonzi kuja Tanzania inaongezeka pamoja kuongeza mashirikiano katika sekta ya biashara ili kuona Kampuni nyingi zaidi kutoka nchi hiyo zinakuja nchini kufanya biashara, ikiwemo uzalishaji wa mbegu pamoja na kusafirisha maua