Media » News and Events

Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania kwenye maeneo yao ya kazi kuangalia zaidi fursa za Uchumi na Maendeleo kwa lengo la kuifanyia kazi kwa vitendo Sera ya mambo ya Nje y

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania kwenye maeneo yao ya kazi kuangalia zaidi fursa za Uchumi na Maendeleo kwa lengo la kuifanyia kazi kwa vitendo Sera ya mambo ya Nje ya Diplomasia ya uchumi.Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo Ikulu, Zanzibar alipozungumza na mabalozi waliofika kumuaga kuelekea kwenye vituo vyao vya kazi.

Dk. Mwinyi aliwaeleza mabalozi hao kuangalia zaidi fursa za uwekezaji kwani Tanzania ina maeneo mengi yanayohitaji wawekezaji hasa baada ya kukutana na wadau wa uwekezaji nchini na kujadiliana nao.Akizungumzia masuala ya Fedha, Rais Dk. Mwinyi aliwataka mabalozi hao kuangalia fursa za mikopo nafuu.

Kuhusu Sekta ya Utalii, Rais Dk. Mwinyi alisema bado Utalii unanafasi pana kwa Uchumi wa taifa kwani unaingiza asilimia 30 ya pato la taifa, hivyo aliwataka mabalozi hao kuongeza jitihada zaidi za kuutangaza kwa wingi Utalii na fursa zilizomo nchini.

Alisema bado nchi inahitaji watalii wengi zaidi ili kukuza Sekta hiyo.Akizungumzia Sekta ya biashara Rais Dk. Mwinyi aliwaeleza mabalozi hao kuangalia fursa kuzitangaza bidhaa zinazozalishwa nchini kwa kuangalia uwezekano wa kuzipatia masoko likiwemo la karafuu na viungo vyengine.

Vilevile, Rais Dk. Mwinyi aliwaeleza mabalozi hao kuendelea kuitangaza Sera ya Uchumi wa Buluu kwani bado kuna maeneo mengi yanahitaji wawekezaji.Akizungumza kwa niaba ya mabalozi wenziwe, Balozi Joseph Sokoine anakwenda kuiwakilisha Tanzania nchini, Canada alimuahidi Rais Dk. Mwinyi kuzifanyia kazi nasaha na miongozo yote aliyowapa kwa nia ya kuziendeleza Sera za Diplomasia ya uchumi na Uchumi wa buluu wa Maendeleo ya taifa.

Mabalozi waliofika hapo ni Balozi Fatma Rajab anaekwenda kuiwakislisha Tanzania nchini Oman, Balozi Naimi Azizi anaekwenda Austria, Balozi Ali Mwadini anakwenda Ufaransa na Balozi Ceasar Waitara anaekwenda kuiwakilisha Tanzania nchini Namibia.Mara baada ya mkutano huo na Mabalozi, Rais Dk.  Mwinyi aliodoka Zanzibar kuelekea Dar es Salaam kwa ziara ya kikazi.