RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje ya Nchi kuhakikisha wanaunga mkono kikamilifu juhudi za Serikali za kutangaza fursa ziliopo nchini ili kuwezesha upatikanaji wa masoko pamoja na kuvutia Wawekezaji.Dk. Mwinyi ametoa wito huo katika Mkutano wa Menejment na Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje ya Nchi, hafla iliofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip, Airpot Zanzibar.
Amesema wakati huu Serikali ikitekeleza Sera ya Uchumi wa Buluu inayohusisha sekta mbali mbali, kama vile Utalii, ujenzi wa Bandari, Uvuvi na Ufugaji wa samaki, kilimo cha mwani, mafuta na gesi pamoja na usafirishaji wa baharini, ni muhimu kwa Mabalozi hao kusaidia juhudi za Serikali ili kupanuwa wigo wa upatikanaji wa masoko pamoja na kuvutia Wawekezaji kutoka maeneo yao ya uwakilishi.Alisema azma ya serikali ni kuhakikisha rasilimali hizo za bahari zinatumika ili kuinua hali za maisha ya Wazanzibari.
Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa Serikali imechukua hatua mahsusi katika kuboresha mazingira ya kibiashara, ikiwa pamoja na kuondoa urasimu katika usajili wa biashara na uwekezaji, sambamba na kuhamisha shughuli za uzalishaji ili kuongeza ajira na mapato.
Alitoa rai kwa Mabalozi hao kuwajengea uwezo watumishi waliopo pamoja na kuwawekea mazingira wezeshi ili waweze kufanya kazi kwa weledi na kuleta ufanisi zaidi.
Aidha, alisema Serikali inaendelea na ujenzi wa miundo mbinu ya barabara katika maeneo maalum ya Uwekezaji pamoja na kuimarisha huduma za umeme na maji pamoja na kuimarisha huduma katika viwanja vya Ndege Unguja na Pemba.
Rais Dk. Mwimyi alisema ni jambo la muhimu kwa Mabalozi hao kujenga mahusiano ya karibu na taasisi za umma na binafsi katika pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili nchi iweze kunufaika na fursa mbali mbali zilioko katika maneeo yao ya uwakilishi.
Aliwataka kuhakikisha vipaumbele vyao vinaendana na vile vivyoko katika mipango ya Serikali zote mbili, huku wakizingatia maelekezo maalum kwa ajili ya Zanzibar, kuambatana na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050, mpango wa maendeleo 2021 – 2026 na Ilani ya CCM ya 2020.
Aidha, Dk. Mwinyi aliwahimiza Mabalozi hao kuendelea kutoa ushirikiano na kufanyakazi kwa karibu na Serikali zote mbili, ili kufanikisha malengo yaliowekwa, ikiwemo upatikanaji wa soko la bidhaa, kutafuta Wawekezaji pamoja na mitaji, sambamba na kuongeza idadi ya watalii watakaozuru nchini.
Nae, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dk. Stergomena Tax amesema kupitia mkutano huo Mabalozi hao walijadili fursa za kiuchumi pamoja na kutembelea miradi mbali mbali ya kimkakati iliotengwa na Serikali ya Mapinduzi ya zanzibar.
Balozi Max alisema kutokana na yale yaliojadiliwa, mkutano huo unalenga kuandaa Mpango kazi ili uweze kuleta tija kwa Taifa.
Alisema Wizara hiyo inaendelea kuhamasisha nchi mbali mbali duniani kufungua Ofisi za Ubalozi hapa Zanzibar na kuzitaja nchi za Falme za Kiarabu , China , India, Msumbiji na Oman kuwa hadi zimekamilisha hatua hiyo.
Aidha, Amidi wa Mabalozi hao Balozi Asha Rose Migiro alisiistiza umuhimu wa kuwekeza katika elimu, akibainisha kuwa hilo ni eneo muhimu sana katika kukuza sekta ya Uchumi wa Buluu.
Mapema, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma Rajabu alisema mkutano huo ilioanza Novemba 14 , 2022 na unaotarajiwa kumalizika Novemba 21,2022 umewahusisha Mabalozi, Ma-konseli wakuu, Menejment ya Wizara, Mwakilishi wa Umoja wa Afrika (AU), ukiwa na maudhui ya kujadiliana, kubadilishana uzoefu, kujadili sera ya Mambo ya nje pamoja na Vipaumbele vya Zanzibar katika utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi