RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka Wazanzibari wote kujitokeza kuhesabiwa katika zoezi la Sensa ya Watu na Makaazi 2022, linalotarajiwa kufanyika Agosti 23, 2022.Dk. Mwinyi ametoa wito huo katika hafla ya makabidhiano ya Anuani za Makaazi, hafla iliofanyika katika makaazi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Migombani, Mkoa Mjini Magharibi.
Amesema Serikali imefikia uamuzi wa kuifanya siku hiyo (Agosti 23, 2020) kuwa ya mapumziko ili kutoa fursa kwa wananchi wote kuweza kushiki kikamilifu katika zoezi hilo litakalofanyika nchini kote.Alisema ana furaha kubwa kupokea anuani hiyo na kufanikisha mchakato huo kwa wakati kabla ya zoezi la sensa na makaazi 2022 kuanza kama ilivyoelekezwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan.
“............... mimi nitashiriki zoezi hilo na matumaini yangu Wazanzibari wote watashiriki zoezi hilo na kumalizika kwa salama na amani”, alisema.
Nae, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Dk. Khalid Salum Mohamed alisema hadi kufikia sasa Wizara hiyo kwa mashirikiano ya karibu na Shirika la Posta Tanzania imefanikiwa kuweka Anuani za Makaazi zipatazo 451,128 Unguja na Pemba, ikiwa ni zaidi ya malengo yaliowekwa.
Alisema hatua hiyo ni ya mafanikio kwa kuzingatia kuwa utekelezaji wake umekwenda sambamba na muongozo wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, alielekeza zoezi hilo liwe limekamilika kabla ya zoezi la sensa ya watu na Maakazi kuanza.
Alieleza kuwa kazi iliobaki ni ya uwekaji wa Vibati katika baadhi ya Nyumba na Majengo, na akabainisha zoezi linaloendelea la uwekaji wa nguzo ambapo nguzo 17,000 zinatarajiwa kuwekwa katika mitaa mbali mbali Unguja na Pemba.
Katika hafla hiyo ambapo Viongozi mbali mbali wa Serikali walishiriki , akiwemo Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita pamoja na Mkuu wa Mkoa Mjini Magahribi Idrissa Kitwana Mustafa; Rais Dk. Mwinyi alikabidhiwa Anwani ya Makaazi Nyumba nambari 78, Wadi ya Migombani, Wilaya Mjini Zanzibar katika Mtaa wa Julius Nyerere Road.
Operesheni ya uwekaji wa Anuani ya Makaazi ilizinduliwa nchini mnamo Februari 8, 2022 na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan, ambapo kwa upande wa Zanzibar ilizinduliwa na Makamo wa Pili wa Rais Hemed Suleiman Abdulla Februari 20,2022.