Media » News and Events

Dk.Hussein Ali Mwinyi ameitaka Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi kuwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti a Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) alipokuwa akizungumza na Viongozi wa Madhehebu ya Dini ya Kikristo katika mkutano uliofanyika leo katika Ukumbi wa Amani Utengamano Welezo Mjini Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameitaka Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi kuwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi itakayobainisha maeneo yaliotengwa kwa ajili ya makaazi pamoja na yale ya ibada.

Dk. Mwinyi ametoa wito huo leo alipozungumza na Viongozi wa Dini ya Kikristo katika mkutano uliofanyika   Kituo cha Amani Utengemano kiliopo Welezo, Mkoa Mjini Maghribi, ambao uliwahusisha Maaskofu, Wachungaji na waumini wa madhehebu mbali mbali wa Dini hiyo, ukiwa na lengo la kuwashukuru wananachi hao baada ya kumchagua kwa kishindo katika uchaguzi mkuu uliopita , sambamba na kusikiliza changamoto zinazowakabili .

Amesema kuwepo kwa mipango bora katika matumizi ya Ardhi kutaondoa changamoto zinazojitokeza za kufanyika ujenzi wa holela wa nyumba za Ibada, ambapo waumini wa dini tofauti hujenga majengo yao katika eneo moja.

Aidha, Dk. Mwinyi aliwataka watendaji wanaoshughulikia utoaji wa vibali vya kazi nchini, kuondokana na urasimu pamoja na utozaji wa gharama kubwa kwa watumishi wa Dini wanaotoka nje na kuja nchini kwa njia ya kujitolea.

Mapema, akisoma Risala ya Baraza la Maaskofu Zanzibar, Mchungaji Shukuru Maloda alisema wakristo wa Zanzibar wanaunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi katika kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani na utulivu, ili kufanikisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.

Nae, Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Zanzibar Agostino Shao ameiomba Serikali kuweka Mawakili wa kushughulikia kesi za Udhalilishaji tangu hatua za mwanzo za upelelezi wa kesi hizo, ikiwa ni hatua ya kuziba mianya kwa jamii kufanya usuluhishi au kuingiza muhali na kuvuruga mustkabali wa kesi hizo