Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amekutana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya FMSS Bilişim Teknolojia ya Uturuki, Ndugu Cihan Aktaş, pamoja na ujumbe wake, waliofika Ikulu Zanzibar leo tarehe 26 Machi 2026.
Rais Dkt. Mwinyi ameihakikishia kampuni hiyo ushirikiano katika kufanikisha dhamira yake ya kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuleta mageuzi ya mfumo wa kidijitali katika sekta ya elimu Zanzibar, na kueleza kuwa elimu ni sekta ya kipaumbele kwa maendeleo ya Zanzibar.
Aidha, ameiagiza Wizara ya Elimu kuendelea na mazungumzo na kampuni hiyo ili kubaini maeneo muhimu ya ushirikiano katika sekta ya elimu, akisisitiza kuwa mbali na kuimarisha elimu, hatua hiyo itaongeza uhusiano mzuri uliopo baina ya Zanzibar na Uturuki.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya FMSS Bilişim Teknolojia ya Uturuki, Ndugu Cihan Aktaş, amesema kampuni hiyo imeamua kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuleta mageuzi katika sekta ya elimu Zanzibar kwa kutumia mfumo wa elimu ya kidijitali. Ameeleza kuwa kampuni hiyo ina uzoefu wa muda mrefu katika mafunzo kwa walimu, teknolojia, ufundishaji na amepongeza hatua iliyofikiwa katika maendeleo ya kielimu Zanzibar
.jpeg)