RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameitaka Wizara ya Ardhi, Nishati na Madini kuanza Programu maalum ya kuhakikisha inatoa Hati miliki katika maeneo yote ya Serikali ili kuzuia uvamizi.Dk. Mwinyi amesema hayo Ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein uliopo Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA) Tunguu katika hafla ya Majumuisho baada ya kukamilisha ziara ya siku mbili katika Mkoa wa Kusini Unguja, ambapo pamoja na kukagua miradi mbali mbali ya maendeleo, pia alipata fursa ya kutembelea na kukagua Miradi mbali mbali inayotekelezwa kwa Fedha za Ahueni ya Uviko -19 pamoja na miradi mingineyo, ikiwemo mradi wa ujenzi Madarsa ya Skuli ya Maandalizi pamoja na skuli ya Msingi uliopo Unguja Ukuu.
Alisema kuna umuhimu wa maeneo yote ya Serikali kupimwa na kupatiwa Hati miliki ikiwa ni hatua ya kuzuia uvamizi, huku akibainisha migogoro ya Ardhi inayowahusisha wananchi na Majeshi ya Ulinzi kuwa tayari imefanyiwa kazi na ripoti yake imeshakabidhiwa Ofisini kwake.Aliipongeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kuja na ubunifu wa kutengeneza Skuli za Elimu Mjumuisho, akibainisha hatua hiyo itatoa fursa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kupata elimu elimu katika amzingira bopra.
Alisema kinachohitajika hivi sasa kinachohitajika ni kupata walimu wenye fani hizo, na akatumia fursa hiyo kumpongeza Mkandarasi w aKituo hicho kwa kazi nzuri..Aidha alishukuru na kutoa pongezi kwa Uongozi wa Mkoa na Kamati ya Ulinzi ya Mkoa huo kwa kuwepo katika hali nzuri ya Ulinzi na Usalama, akibainisha hilo ni jukumu kubwa la Uongozi wa Mkoa.
Aidha, aliyashukuru mabaraza ya mji na kusema amekoshwa na mabaraza ya mkoa huo kwa utekelezaji wa maagizo yake aliyoyatoa katika ziara iliopita, huku akitoa rai ya kuwataka kuongeza bidii katika makusanyo pamoja na kuongeza kiwango cha kuelekeza kwenye maendeleo.Alitumia fursa hiyo kuwapongeza Wakandarasi wa Hospitali zote mbili ziliomo Mkoani humo kwa kufanya vizuri katika ujenzi na kubainisha azma ya serikali ya kuendleea kuwapa kazi wazawa, kwani hatua hiyo itabakisha fedha kwenye mzunguko nchini.
Aidha, Aliitaka Wizara Afya kujipanga kwa kuweka mazingira bora ya Hospitali hizo ili kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa maji ya uhakika pamoja na Vifaa Tiba ili kupunguza kiwango cha wagonjwa kwenda Mnazi Mmoja.Aidha, Dk. Mwinyi aliupongeza Uongozi wa Mkoa huo kwa kujenga vituo bora vya wajasiriamali, ikilinganishwa na Mikoa mingine, huku akilipongeza Jeshi la Zimamoto kwa weledi wa kazi yao.
Sambamba na hilo, Dk. Mwinyi alisema wakati wa kampeni wajasiriamali walipewa ahadi ya kuwekewa mazingira bora ya kufanyia biashara zao, elimu, mitaji pamoja na masoko, hivyo kinachohitajika ni wao wenyewe kuchangamkia fursa iliopo.Katika hatua nyengine Dk. Mwinyi aliiagiza Wizara ya Uchumi wa Buluu kutafuta njia za kujenga Bandari za Uvuvi pamoja na kujenga viwanda vya kusindika samaki ili kuwawezesha wavuvi kupata soko la uhakika.
Alisema Barabara ya Tunguu – Makunduchi tayari Serikali imeshapata fedha na hivi karibuni Serikali itatiliana mkataba kwa ajili ya ujenzi wA barabara hiyo.
Aliushukuru Uongozi wa Mkoa na Wilaya hiyo kwa maandalizi mazuri ya ziara hiyo pamoja na kuwashukuru Viongozi na wananchi wote walioshiriki katika ziara hiyo.
Nae, Mkuu wa Mkoa huo Hadidi Rashid Hadid alisema Mkoa huo una utulivu mkubwa wa kisiasa, sambambamba na Uongozi wa Mkoa kupata mashirikiano makubwa kutoka kwa Viongozi wa Chama na Serikali Mkoani humo.