RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuipatia vyenzo zote zinazohitajika Skuli ya Sekondari Mtule ili wanafunzi waweze kupata elimu bora.Dk. Mwinyi ametoa wito huo huko Mtule Mkoa wa Kusini Unguja katika uzinduzi wa Skuli ya Sekondari Mtule, baada ya kufanyiwa ukarabati mkubwa kufuatia changamoto kadhaa zilizokuwa zikiikabili skuli hiyo, ikiwemo madarasa yake kuvuja.

Amesema kuna umuhimu wa Wizara hiyo kuipatia vifaa na nyenzo skuli hiyo, ikiwemo Komputa pamoja na uzio ili wanafunzi waweze kupata elimu bora na sio bora elimu.Aidha, aliitaka Wizara hiyo kuangalia uwezekano wa skuli hiyo kujenga Dahalia la wavulana, hatua inayotokana na azma ya mkandarasi wa ujenzi huo Kampuni ya kujenga Dahalia la wasichana yenye uweo wa kuchukua wanafunzi 80.

Rais Dk. Mwinyi aliwataka watendaji kuzingatia wajibu wao wa kusimamia vyema wakati wanapotoa zabuni kwa miradi mikubwa ili hatimae waweze kupata kazi inayokidhi vigezo.Alisema ukarabati mkubwa wa Skuli hiyo usingelifanyika kama watendaji hao wangezingatia wajibu wao wakati walipotoa zabuni ya ujenzi wa skuli hiyo kwa mara ya kwanza, jambo liloilazimu Serikali kutumia fedha za ziada na kutoa indhari ya jambo hilo kuwa funzo kwa watendaji hao.

Aidha, Dk. Mwinyi alipongeza matokeo ya Mitihani hiyo ya kidato cha sita mwaka huu, akibainisha kuwa yamekuwa mazuri mno.

Mapema, Rais Dk. Mwinyi alishiriki katika hafla ya makabidhiano ya Maboti pamoja na Bajaji kwa Wavuvi , Wakulima wa Mwani na Bajaji kwa Wajasiriamali wa Wilaya Kusini Unguja, katika hafla iliofanyika Paje Mkoa Kusini Unguja.Alisema makabidhiano hayo ni utekelezaji wa ahadi aliyotoa wakati wa Kampeni za uchaguzi Mkuu wa 2020 zilizolenga kuwapatia vifaa vya kisasa wananchi ili kuendeleza shughuli zao, na hivyo akatumia fursa hiyo kuwataka kuanza kuzitumia vifaa hivyo.

Alisema Serikali iko tayari kutoa Maboti makubwa kwa wananchi hao,ila kinachohitajika ni kuhakikisha wanaweza kurejesha fedha walizokopa, ambazo zinalipwa bila riba.Alipongeza kazi za kuleta maendeleo kuwa zinaendelea vizuri na wale waliopewa majukumu wanafanya vyema.

Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kujiunga katika vikundi na kufika katika Ofisi za Mikoa na Wilaya kwa ajili ya kupata utaratibu wa kupata mikopo hiyo.

Nae, Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Suleiamn Masoud alisema Mkoa wa Kusini Unguja umepata jumla ya Maboti 77 ya Uvuvi, Maboti 75 kwa ajili ya Vikundi vya Mwani , ambapo matarajio ni kuzalisha ajira zipatazo 5,000. 

Ziara ya Rais Dk. Mwinyi itaendelea kesho kwa kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo katika Wilaya Kati Unguja.