RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amekemea tabia ya baadhi ya viongozi wa Serikali, majimbo, wakuu wa Mikoa, Wilaya na viongozi wa halmashauri kutoelewana kwenye utendaji kazi wao.Alisema, hali hiyo inayodhorotesha utendaji na maendeleo ya Serikali, mikoa na halmashauri kwa baadhi ya viongozi hao kutoelewana.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo Ikulu, Zanzibar, alipowaapisha wakuu wa Mikoa wawili na wakuu wa Wilaya watatu aliowateua hivi karibuni.Pia, Rais Dk. Mwinyi aliwaonya baadhi ya viongozi wasioshughulikia kero za wananchi na wale wanaojihusika na kero hizo na kuwataka wafanyekazi ya kuwatumikia wananchi kwa kutenda haki badala ya kuwa sehemu ya kero hizo.

“Kazi yenu kuhakikisha mnasikiliza kero za wananchi kwenye maeneo yenu, wananchi wanachangamoto nyingi, kabla ya kuzifikisha ngazi za juu mhakikishe kwenu nyinyi zimeshindikana” alinasihi Rais Dk. Mwinyi.Akizungumzia migogoro ya ardhi, Rais Dk. Mwinyi amesema imekua tatizo kubwa hasa kwa baadhi ya viongozi kujihusisha na kero hizo, hivyo, aliiwaasa viongozi hao kuhakikisha wanatatua kero hizo na kutenda haki kwa wananchi sio kuwaachia hadi kufikisha malaalmiko yao kwa ngazi za juu za Serikali.

Kuhusu kero za wawekezaji alitumia fursa hiyo kuwataka Wakuu hao wa Mikoa na Wilaya kutatua kero za wawekezaji kwenye ngazi zao kwa kuwatendea haki sio kuwapendelea au kuwadhulumu.Pia, aliwataka Wakuu wa Mikoa na wilaya kusimamia vema waliochini yao hususani halmashauri za wilaya na manispaa zao hasa kwa wajasiriamali wadogo na kushughulikia suala la usafi wa mazingira badala ya kuiachia serikali kuu.

Halkadhalika Rais Dk. Mwinyi alikemea uhusiano mbaya baina ya Viongozi wa Serikali, mikoa, wilaya wakiwemo pia na mawaziri, wawakili na wabunge majimboni pamoja na wakurugenzi wa halmashauri.Aliwataka viongozi wote kufanya kazi pamoja, kushirikiana na kuelewana, na kuwaonya tabia ya kususiana kwenye majukumu yao, suala linalodhorotesha utendaji kazi Serikalini na akaonya iwapo hapana budi ya kuacha tabia hiyo atachukua hatua.

Rais Dk. Mwinyi aliwataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote za Zanzibar kuhakikisha wanatoa kipaumbele kwenye suala la ulinzi na usalama katika maeneo yao.Alisema kuna baadhi ya maeneo hayo kumeripotiwa matukio mengi ya uvunjifu wa amani hasa maeneo ya Paje Mkoa wa kusini Unguja na Nungwi, Kaskazini Unguja hivyo aliwataka viongozi hao kuyashughulikia matukio hayo kwa nguvu kubwa na kuendesha operesheni maalum ya kudhibiti hali hali hiyo isitokee kwenye maeneo hayo ambapo Serikali imeweka nguvu kubwa ya Utalii.

Walioapishwa ni Mhe. Ayoub Mohamed Mahmoud kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja awali alikua Mkuu wa Kaskazini Unguja, Mhe. Rashid Hadid Rashid kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja awali alikua Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja.Wengine ni Mhe. Sadifa Juma Khamis kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kati, mkoa wa Kusini Unguja kabla alikua Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A Unguja.

Halkadhalika, Rais Dk. Mwinyi amemuapisha Othman Ali Maulid kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A Unguja awali alikua Mstaafu kutoka Utumishi wa Umma.Pia Rais Dk. Mwinyi amemuapisha Galos Nyimbo kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja kabla ya hapo Galos alikua mwanajeshi Mstaafu.Viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali, viongozi wa Dini na Vyombo vya ulinzi na usalama pia walihudhuria hafla hiyo.