Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Watanzania wataendelea kumkumbuka na kumuenzi Hayati Dk. John Pombe Magufuli kwa kuendeleza falsafa na maono yake pamoja na mambo mazuri yote aliyoyafanya kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo huko katika katika uwanja wa Magufuli Chato, wakati akitoa hutuba yake katika Kumbukizi ya mwaka mmoja wa kifo cha Hayati Dk. John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tukio lililoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambalo liliambatana na Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Baba Askofu Flavian Mkatala.
Rais Dk. Mwinyi ambaye amefuatana na Mama Mariam Mwinyi, alisema kuwa Watanzania wataendelea kukumbuka uongozi wa Hayati Dk. John Pombe Magufuli uliokuwa umetawaliwa na busara, umahiri na ujasiri.
Katika hotuba yake hiyo, Rais Dk. Mwinyi aliwafikishia wanafamilia, ndugu, jamaa, marafiki, Wananchi wa Chato na Watanzania wote salamu za upendo kutoka kwa Wananchi wa Zanzibar.
Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa kutokana na alama alizoziacha Marehemu Rais Magufuli kwa maendeleo ya Taifa pamoja na namna kifo chake kilivyogusa na kusononesha nyoyo za Watanzania, inaonekana kama vile kifo chake kimetokea wiki chache zilizopita, na siyo mwaka mmoja uliopita kama ilivyo katika uhalisia.
Alisema kuwa kwa hakika Watanzania wataikumbuka kwa majonzi makubwa siku kama hii ya leo, ya tarehe 17 Machi mwaka jana, wakati walipopokea kwa mshutuko taarifa ya kifo chake na majonzi makubwa wakati wa kufanya Mazishi yake hapa Chato tarehe 26 Machi, 2021.
“Tutaendelea kujifunza kutokana na historia yake kwa kutumia nadharia mbali mbali alizotuachia katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na ustawi wa Jamii”,alisema Rais Dk. Mwinyi.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa wakati Hayati Rais Magufuli anakumbukwa na kuenziwa na kumuombea dua, Watanzania wanamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwapa mrithi madhubuti, shupavu, mwenye nia thabiti, uono na ujasiri wa kuendeleza mambo mazuri aliyoyaacha Marehemu pamoja na viongozi wengine wa Taifa letu wa Awamu zilizotangulia katika pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa kauli mbiu aliyokuja nayo baada ya kurithi kiti cha Marehemu inayosititiza kwamba ‘KAZI IENDELEE’ ni ushahidi wa dhamira yake ya kuendeleza mambo mazuri yaliyoachwa na Marehemu pamoja na viongozi walioongoza kabla yake.
Hivyo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa ni jukumu la Watanzania wote kuendeleza kazi hiyo kwa kadri ya uwezo wa kila mtu nan i wazi kuwa kauli mbiu hiyo ni njia bora ya kumuenzi Marehemu Dk. John Pombe Magufuli ikiwa leo inatimia mwaka mmoja tokea kifo chake.
Aliongeza kuwa njia bora kwa Watanzania ni kuendelea kuchapa kazi kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji, uzalendo na uadilifu.
“Kwa umoja wetu, tuna jukumu la kukuhakisha kwamba tunaendelea kumuenzi Marehemu kwa kupiga vita vitendo vya rushwa, ufisadi, uzembe na ubadhirifu wa mali ya umma, mambo ambayo aliyasimamia kwa nguvu zote wakati wa kipindi chake cha uongozi,”alisisitiza Rais Dk. Mwinyi.
Alisisitiza kwamba kazi iendelee kwa kuendeleza yote mazuri yaliyofanywa na Marehemu katika masuala muhimu na mazito yanayohusu maendeleo na kuendelea kuhakikisha kuwa kunakuwa na matumizi bora na endelevu ya rasilimali zilizopo.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alisisitiza kumkumbuka Marehemu Rais Magufuli kwa kuendeleza misingi ya umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa Watanzania bila ya kubaguana kwa kabila zetu, dini zetu, rangi au sehemu tunazotoka.
“Tuendeleze kazi ya kuzidumisha, kuzitangaza, kuzipenda na kuziendeleza tamaduni zetu pamoja na kufanya kazi kubwa ya kuitangaza na kuieneza lugha ya Kiswahili duniani kote, kama aliyoturithisha Marehemu na wengine waliotangulia”,alisisitiza Rais Dk. Mwinyi.
Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi akiwa amefuatana na Mama Mariam Mwinyi alifika katika kaburi la Hayati Dk. John Pombe Magufuli na kuweka shada la maua na kutia saini kitabu cha maombolezi pamoja na kumsalimia mama wa Hayati Magufuli.