Media » News and Events

Dk.Hussein Ali Mwinyi ametembelea maonyesho ya Saba ya Biashara Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametembelea maonyesho ya Saba ya Biashara Zanzibar na kuridhia ombi la wafanyabiashara la kuongezewa siku mbili zaidi.Akizungumza na uongozi wa Wizara ya Biashara pamoja na Kaimu Waziri wa Wizara hiyo ambaye pia ni Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji Mudrik Soraga, kabla ya kutembelea maonyesho hayo alisema kuwa si vibaya maonyesho hayo ya biashara yakaendelea kwa siku mbili na badala yake yakafungwa Jumaapili ya Januari 17 badala ya Ijumaa ya Januari 15 kama ilivyopangwa.

Akitembelea maonyesho hayo, Rais Dk. Mwinyi ambaye alikuwa amefuatana na Mama Mariam Mwinyi alivutiwa na biashara mbali mbali zinazouzwa na wafanyabiashara kadhaa wakiwemo wajasiriamali wa ndani na nje ya Zanzibar na kusisitiza haja ya Wizara husika kuendelea kuwaunga mkono.Rais Dk. Mwinyi pia, alitumia fursa hiyo kuwasikiliza wajasiriamali mbali mbali aliowatembelea kwa niaba ya wenzao mafanikio waliyoyapata katika shughuli zao pamoja na changamoto walizonazo wakati wa maonyesho hayo na katika shughuli zao wanazozifanya.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi aliwaahidi wafanyabiashara wakiwemo wajasiriamali hao kwamba atahakikisha changamoto zao zinazowakabili zitafanyiwa kazi kwa lengo la kupata mafanikio zaidi.Mapema Waziri wa Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji Mudrik Soraga alimueleza Rais Dk. Mwinyi Taasisi zilizoshiriki katika maonyesho hayo ni 360 zikiwemo zile za ndani na nje ya Zanzibar.

Alieleza kuwa maonyesho hayo ambayo yalizinduliwa rasmi Januari 6, 2021 na Makamo wa Rais wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, zimeshirikisha taasisi hizo 360 zikiwemo 340 za Wajasiriamali na 12 za kifedha miongoni mwa Taasisi hizo.Aidha, Waziri huyo alimueleza Rais Dk. Mwinyi shughuli mbali mbali zilizofanyika katika maonyesho hayo ya Saba ambayo yalitarajiwa kufungwa Januari 15 lakini wafanyabiashara wameleta ombi maalum la kuongezewa siku mbili na badala yake walitaka lifungwe Januari 17 siku ya Jumaapili ambalo Rais Dk. Mwinyi ameridhia.

Rais Dk. Mwinyi akiwa na Mama Mariam Mwinyi walitembelea katika mabanda mbali mbali ya maonyesho ya biashara yakiwemo ya wajasiriamali kama vile yanayohusiana na masuala ya mwani, viatu, vifaa vya ujenzi, mazulia, ujasiriamali wa vikundi vya watu wenye ulemavu na mabanda mengineyo.

Nao wafanyabiashara hao walimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa hatua yake hiyo ya kwenda kuwatembelea sambamba na kumueleza changamoto na mafanikio wanayoyapata.

Maonyesho hayo ya biashara ambayo hufanywa kila mwaka katika shamrashamra za sherehe za Mapinduzi ya Januari 12, 1964 kwa mwaka huu yatakuwa ni ya saba tokea kuasisiwa kwake.