Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam H. Mwinyi, ambaye pia ni Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), ameendelea kuonesha uongozi thabiti katika kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia. Kampeni hii inalenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu athari za ukatili wa kijinsia, njia za kujilinda, na umuhimu wa kuchukua hatua za pamoja kukomesha tatizo hili.

Takwimu za mwaka 2024 zinaonesha ukubwa wa changamoto hii, ambapo jumla ya kesi 1,809 za ukatili wa kijinsia ziliripotiwa nchini, na kati ya hizo 1,525 zilihusisha watoto. Hali hii inathibitisha haja kubwa ya kuendeleza juhudi, kuimarisha ulinzi wa watoto, na kuhakikisha jamii inasalia makini dhidi ya vitendo vyote vya ukatili.

Leo tarehe 03 Desemba 2025, Mama Mariam alishiriki katika shughuli za kampeni kwa kuwatembelea Vijana wa Makachu pamoja na wakina mama wajasiriamali wa Forodhani, Mkoa wa Mjini Magharibi. Ziara hii imeongeza ari ya ushirikiano na kuonyesha msimamo wa pamoja wa kulinda haki, utu na ustawi wa wanawake, watoto na jamii nzima.

Akiwa ameambatana na Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya ZMBF, Afisa Mtendaji Mkuu, na watumishi wa Taasisi, Mama Mariam alisisitiza dhamira ya pamoja ya kutokomeza ukatili wa kijinsia, sambamba na ujumbe wa No More Campaign unaohimiza jamii kusimama na kusema, “Hapana Tena kwa Ukatili.”

Kampeni ya Siku 16 inaendelea kuwa jukwaa muhimu la kuhamasisha, kuelimisha na kuimarisha mshikamano wa wananchi katika kupinga ukatili, na kujenga jamii salama, yenye usawa na haki kwa wote.