MKE wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mama Mariam Mwinyi ameitaka jamii kuwaangalia kwa jicho la huruma na kuwasaidia watoto yatima wanaoishi na virusi na Ukimwi (VVU) katika kituo cha ‘ZASO Children Home’ kiliopo Fuoni Mambosasa, Mkoa Mjini Magharibi.

Mama Mariam Mwinyi ametoa wito huo wakati alipofika kituoni hapo kwa ajili ya kukabidhi sadaka za Iftar kwa watoto hao, ikiwa ni muendelezo wake wa kukabidhi sadaka kwa wananchi wa makundi mbali mbali katika Mikoa ya Unguja na Pemba.

Amesema kuna umuhimu mkubwa kwa jamii ya Wazanzibar, hususan watu wenye uwezo kuguswa na uwepo wa kituo hicho na kuwaangalia kwa jicho la huruma watoto waliopo kwa kuwasaidia ili waweze kukua vyema.

Alisema pale watoto hao watakapopata lishe bora, uangalizi pamoja na matibabu hakuna sababu ya wao kushindwa kufikia malengo yao ya kimaisha.

Alitumia fursa hiyo kuwatakia swaumu na sikukuu njema ya Idd el Fitri, huku akiwaahidi kukutana nao siku ya sikukuu itakapofika.

Nae, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Vijana na Watoto Anna Paul alimshukuru Mama Mariam kupitia taasisi ya ‘Zanzibar Maisha Bora Foundation kwa hatua yake ya kuwasaidia wananchi wa makundi mbali mbali , sambamba na kumuomba awe mlezi wa watoto katika Kituo cha ‘ZASO Children Home’.

Katika hatua nyengine kwa nyakati tofauti; Mama Mariam Mwinyi alipata fursa ya kukabidhi sadaka mbali mbali, ikiwemo mafuta ya kupikia, mchele, unga ngano, tende pamoja na Sukari kwa wananchi wa makundi mbali mbali katika shehiya za Bumbwini Mafufuni, Makoba, Matemwe Kijini, Mbuyu Tende pamoja na Kijibwe mtu.


Katika salamu zake kwa wananachi hao, alisema amefarijika sana na muitikio wao na kubainisha namna Serikali inavyowapenda wananchi wake, ikiwemo kundi la wazee kwa kuamini kuwa wanahitaji matunzo.

Mapema, Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja Rashid Hadidi Rashid aliwashukuru wananchi wenye uwezo kwa hatua yao ya kuitikia wito wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mpinduzi Dk. Hussein Mwinyi wa kuwaisidia wananchi wenye uwezo duni, hususan katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Aidha, Mkuu wa Mkoa Kaskazini Unguja, Ayoub Mohammed Mahamoud alimshukuru Mama Mariam Mwinyi kwa hatua yake ya kuendeleza utaratibu wa kuwasaidia wananchi sadaka mbali mbali, hatua iliowawezesha wananchi wa Shehiya za Matemwe Kijini na Mbuyu Tende na o kunufaika. 

Kw aupande wake, Mohamed Salum akitoa shukurani kwa niaba ya wananchi wa Shehiya ya Kijibwemtu alimshukuru Mama Mariam kwa kusaidia upatikanaji wa sadaka hiyo, sambamba na kuishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kusimamia suala la amani na hivyo kuwezesha kufanyika shughuli mambli mbali za kijamii.