Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema michezo ni nyenzo muhimu na alama ya kuwaunganisha watu wa jamii na mataifa mbalimbali katika kuimarisha ushirikiano, upendo na umoja. Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 24 Disemba 2025 alipolifungua Tamasha la Michezo la Zanzibar Sports Festival, linalofanyika katika Viwanja vya Maisara Sports Complex, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Ameeleza kuwa kufanyika kwa mashindano hayo hapa Zanzibar ni tukio la kihistoria na kumbukumbu muhimu kwa Jumuiya ya hoja Shia Ithnashir, ambayo yalianzishwa nchini miongo kadhaa iliyopita. Dkt. Mwinyi amesema Zanzibar inajivunia kuona mashindano hayo yakifanyika kwa mara ya kwanza huku yakishirikisha wanamichezo wapatao 300 kutoka jumuiya mbalimbali za Khoja Shia Ithnashir duniani, wakiwemo wanaume na wanawake, hatua aliyoielezea kuwa ni jukwaa muhimu la kuleta furaha, upendo, mshikamano na kukuza michezo.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amefahamisha kuwa michezo, mbali na kuleta burudani, hufundisha nidhamu, heshima na udugu, na ni kichocheo cha ushirikiano miongoni mwa jamii, akisisitiza kuwa ni fursa ya kukuza uchumi, biashara, usafirishaji na kuibua fursa mbalimbali kwa wananchi. Rais Dkt. Mwinyi ametoa wito kwa wanamichezo hao kushiriki mashindano hayo kwa kuonesha upendo, uhusiano mwema na udugu baina yao, ili kuyafanya mashindano hayo kuwa ya mafanikio, sambamba na kutumia fursa ya kutembelea vivutio vya utalii na maeneo ya kihistoria ya Zanzibar.

Ameipongeza Taasisi ya Africa Sports Federation kwa kuandaa semina ya wawekezaji itakayojadili fursa za kiuchumi na uwekezaji zilizopo Zanzibar kwa wageni wanaoshiriki mashindano hayo kutoka mataifa mbalimbali, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha uchumi, maendeleo na ushirikiano wa kimataifa wa kiuchumi.

Mapema, Katibu wa Jumuiya ya Islam Jammat ya Zanzibar, ambayo ndiyo mwenyeji wa mashindano hayo, Ndg. Hassan Mohamed Raza, amesema kufanyika kwa mashindano hayo Zanzibar kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuwepo kwa miundombinu ya kisasa ya michezo, ikiwemo viwanja bora vya michezo mbalimbali, na akampongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa dhamira na nia yake ya kuinua sekta ya michezo nchini.

Mashindano hayo ya 47 ni ya kwanza kufanyika Zanzibar tangu kuanzishwa kwake zaidi ya miaka 150 iliyopita, yakiwakutanisha jumuiya za Majamati 34 kutoka nchi mbalimbali duniani.