Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi ametoa shukurani kwa Taasisi ya Ahmad Mohamed Al Falasi kwa misaada waliyoitoa kwa ajili ya wananchi wenye mahitaji maalum katika kipindi hichi cha kuelekea mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Akipokea misaada hiyo ikiwemo vyakula, mafuta ya kula, tende, misahafu, dawa kwa ajili ya akina mama na watoto huko Ofisini kwake Migombani, Mama Mariam Mwinyi alieleza kuwa atahakikisha misaada hiyo inawafikia walengwa.

Mama Mariam Mwinyi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya ‘Zanzibar Maisha Bora Foundation’ (ZMBF), alitumia fursa hiyo kuishukuru na kuipongeza Taasisi ya Ahmad Mohamed Al Falasi kwa misaada iliyoitoa ambayo alisema imekuja wakati muwafaka ambapo wananchi wa Zanzibar wamo katika maandalizi ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Nae kiongozi wa Taasisi hiyo, Sheikh Ahmad Mohamed Al Falasi kutoka Falme za Kiarabu (UAE), alimuhakikishia Mama Mariam Mwinyi kwamba Taasisi yake itaendeleza utamaduni huo ili kuhakikisha wale wenye mahitaji maalum wanapatiwa misaada hiyo hasa katika kipindi hichi cha kuelekea mwezi Mtukufu wa Ramadhani