MKE wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mama Mariam Mwinyi amewataka watoto Yatima pamoja na wanaoishi katika mazingira magumu kuendeleza mambo mema waliyojifunza katika mwezi mtukufu wa Ramadhani , sambamba na kumcha Mwenyezi Mungu kwa kudumisha ibada.

Mama Mariam ametoa wito huo kwa nyakati tofauti alipotembelea Vituo vinavyolea na kutunza watoto yatima pamoja na wanaoishi mazingira magumu kwa ajili ya kutoa mkono wa Idd el Fitri.

Katika ziara hiyo Mama Mariam alivitembelea Vituo vya ZASO Children Home, SOS pamoja na Mazizini, Mkoa Mjini Magharibi. 

Amesema katika mwezi wa Ramadhani watoto hso waliweza kujifunza mambo mengi mema, hivyo akatumia fursa hiyo kuwataka waendele na tabia njema pamoja na kufanya Ibada, hususan katika kadumisha sala.

Aidha, aliwatakia sikukuu njema watoto hao, huku akiwasisitiza umuhimu wa kuzingatia usalama wao katika kipindi chote cha sikukuu, hususan wawapo barabarani.

Alisema katika kipindi kama hiki, watu waovu hukitumia kwa ajili ya kufanikisha malengo yao, hivyo wanapaswa kuchukua tahadhari wanapokwenda kwenye viwanja vya sikukuu.

“Mnapaswa kuchukua tahadhari mnapokwenda kwenye maeneo ya sikukuu, muwe waangalifu muwapo barabarani na msiongee na watu msiowajua,wale watoto wakubwa wanatakiwa kufuatana kwa makundi na wale wadogo ni lazima waambatane na wazazi au walezi wao”, alisema.

Vile vile Mma Mariam aliwakumbusha watoto hao umuhimu wa kuzingatia masomo yao ili kufikia ndoto zao katika maisha.

Nae, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Riziki Pembe Juma alimweleza Mama Mariam jinsi jamii ikiwemo watoto invyofarijika na ya yale anayoyafanya, ikiwa pamoja na kuwajali na kuwapenda watoto.

Akizungumza kwa niaba ya Mama Mariam, kwa nyakati tofauti alipotembelea alipotembelea vituo vya Kuhudumia wazee vya Welezo na Sebleni, Waziri Pembe alisitiza umuhimu wa wazee hao kuendelea kufanya mambo mema ikiwemo ibada kama ilivyokuwa katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Aidha, aliwataka wazee hao kumuombea Dua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi pamoja na familia yake ili aweze kutekeleza vyema majukumu yake ya kitaifa.

Nae, Mkurugenzi Ustawi wa Jamii na Watoto Abdalla Saleh Omar, alisema hatua ya mama Mariam kutembeela vituo hivyo kwa ajili ya kutoa mkono wa Eid el Fitri ni uthibitisho kwa kiasi gani kiongozi huyo anavyowajali wazee, ikiwa ni utekelezaji wa malengo ya Mapinduzi ya 1964.

Mapema, akitoa shukrani kwa niaba ya watoto wa Kituo cha ZASO Children Home Amina Abdillah alisema watoto wa kituo hicho wamefarijika mno na hatua ya kiongozi huyo ya kuwatembelea na kutoa mkono wa Eid el Fitri, na hivyo akamtakia kheri nyingi kwa Mweneyzi Mungu kutokana na upendo mkubwa anaouonyesha juu yao.